1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Kenya kuwahamisha raia wake waliokwama Sudan

Wakio Mbogho18 Aprili 2023

Serikali ya Kenya inafanya mipango ya kuwahamisha raia wake wanaoishi Sudan kufuatia mapigano yanayoendelea nchini humo yaliosababisha vifo vya takriban watu 200.

https://p.dw.com/p/4QFvd
Kämpfe im Sudan
Picha: Marwan Ali/AP/picture alliance

Hali nchini Sudan imesalia kuwa tete huku mapigano kati ya majeshi ya serikali na ya waasi yakiendelea mjini Khartoum na hata kuenea hadi kwenye uwanja wa ndege na eneo la bandarini. Ni kwa sababu hiyo serikali ya Kenya inawahimiza Wakenya walioko maeneo yanayoshuhudia vurugu nchini Sudan kusalia majumbani mwao. Katibu mkuu wa wizara ya masuala ya kigeni Roselyn Njogu ametoa tangazo hili. "Tumejitolea kuhakikisha kwamba Wakenya wote wameokolewa na kurejeshwa nyumbani iwapo hilo litahitajika. Tunawahimiza Wakenya wote walioko Sudan kusalia ndani ya nyumba."

Soma pia: Guterres ataka kusitishwa mapigano nchini Sudan

Sudan RSF Lieutenant General Mohamed Hamdan Dagalo
Pande hasimu zimekubaliana kusitisha mapigano kwa mudaPicha: Umit Bektas/REUTERS

Wizara ya masuala ya kigeni ya Kenya imesema kuna takriban Wakenya elfu tatu wanaoishi na kufanya kazi nchini Sudan. Kufikia sasa hakuna yeyote kati yao aliyejeruhiwa, lakini imetoa nambari ya mawasiliano ya dharura kuwawezesha kuufikia ubalozi wa Kenya mjini Khartoum wanapoitaji msaada wowote wa kibinadamu. "Tuna karibu wanafunzi 400 walio Sudan. Tuna idadi kubwa ya Wakenya wanaofanya kazi katika mashirika ya kimataifa nchini humo pia tunao wafanyakazi wa majumbani. Tunaendela na mchakato wa kujumuisha idadi yote ya Wakenya walioko Sudan ndio maana tumewahimiza Wakenya kuwasiliana na ubalozi.”

Kwa mujibu wa Volker Perthes, mwakilishi maalum wa Umoja wa mataifa nchini Sudan, mapigano hayo ambayo yameendelea kwa siku nne sasa yamesababisha vifo vya watu zaidi 180 na wengine 1,800 kujeruhiwa.

Shirika la madaktari wasio na mipaka MSF limeeleza kwamba watu wengi wakiwemo wahudumu wa afya wamekwama. Kituo cha MSF eneo al Nyala Sudan Kusini kilivamiwa na kuporwa. Hospitali zote zilizoko eneo la Sudan Kaskazini zimelazimika kufunga, baadhi kwa kwa sababu ya ukaribu na mapigano na nyengine kwa ajili ya kukosa wahudumu wa afya watakaowahudumia manusura. Martha Kihara, mshauri wa matibabu wa Sudan katika shirika la MSF anasema pale ambapo wameweza kutoa huduma ya afya hali ni mbaya.

Anafahamisha kwamba wengi wa wale ambao wameweza kuwatibu ni raia hasa watoto. Matabibu wa MSF wana wasiwasi kwamba vifaa vya matibabu, madawa na damu kwenye hospitali vinaisha. Kumekuwa na hali ya umeme kupotea tangu mapigano yalipoanza jumamosi. Mafuta ya jenereta ya hospitali pia yanaisha. Kutokana na uhasama huo uwanja wa ndege na njia zingine za usafiri zimekatishwa. Mjini Khartoum hata magari ya wagonjwa hayaruhusiwi kupita ili kuokota miili ya waliofariki iliyotapakaa mitaani.

Wadau hao wametoa wito kwa maafisa wa afya na wagonjwa wasilengwe bali waruhusiwe kusafiri ili maisha yaweze kuokolewa.

Wakio Mbogho, DW, Nakuru.