1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kutupa dozi 800,000 za Covid-19 zilizoisha muda

24 Machi 2022

Wizara ya afya nchini Kenya imetangaza kwamba muda wa matumizi wa zaidi ya dozi laki nane dhidi ya ugonjwa COVID-19 aina ya AstraZeneca umekamilika bila kutumiwa.

https://p.dw.com/p/48y2a
Vernichtung von Corona-Impfdosen
Picha: Kola Sulaimon/AFP/Getty Images

Idadi ya watu wanaojitokeza kuchanjwa imepungua pakubwa baada ya serikali kulegeza baadhi ya masharti yaliyowekwa kudhibiti janga la virusi vya corona, hasa kuondolewa kwa sharti la kuvaa barakoa maeneo ya umma.

Sababu iliyotolewa ya kuharibika kwa chanjo ya AstraZeneca ambayo muda wake wa kutumika umekamilika ni kama vile, hatua ya Wakenya kusuasua kupokea chanjo hasa baada ya kuondolewa kwa sharti la kuvaa barakoa kwenye maeneo ya umma, baadhi ya watu wametaka kuchagua chanjo moja dhidi ya nyingine, na pia kumekuwa na uenezaji wa habari potofu kuhusu chanjo ya COVID-19.

Daktari Willis Akwale, ni naibu mwenyekiti wa jopo kazi linalosimamia masuala ya chanjo nchini.

"Kufikia Februari, 28 dozi 843,000 za Astrazeneca hazikuwa zimetumika kumaanisha sasa zimeharibika. Tulipata taarifa hii yote wiki iliyopita baada ya kukusanya ripoti kutoka kaunti zote. Kati ya dozi hizi, takriban dozi 570 zilikuwa katika vituo vya maeneo tofauti nchini tayari kutumika.”

Weltspiegel 05.03.2021 | Corona | Kenia Nairobi | AstraZeneca-Impfstoff
Chanjo za Covid-19 zilizopelekwa eneo la Kitengela, KenyaPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Kila kaunti ilirekodi kuwa na chanjo zilizokamilika muda, Nakuru ikirekodi idadi kubwa zaidi ya dozi 35,790. Ilikufuatiwa na Busia ikiwa na idadi ya dozi 27.980 na Kajiado ikirekodi dozi 25,770. Kadhalika, dokta Akwale anaonya kuwa dozi milioni moja nukta moja za chanjo aina ya Johnson and Johnson huenda muda wake wa matumizi ukakamilika iwapo hazitatumika kufikia tarehe 15 mwezi Aprili.

Hata hivyo Dokta Daniel Wainaina afisa mkuu wa afya ya umma katika kaunti ya Nakuru anasisitiza kuwa ni kiasi kidogo cha chanjo zilizoharibika ikilinganishwa na zile zilizotumika. Vilevile, amesema kaunti ya Nakuru inazo juhudi kufikia idadi inayolengwa ya watu waliochanjwa.Kenya yaondoa masharti ya mwisho ya Covid-19

Wizara ya afya nchini inasikitishwa na mwelekeo huu, inapotafakari juhudi zilizowekwa katika kuzipata chanjo hizi za COVID-19. Ili kupunguza visa vya kuharibika kwa chanjo zaidi, wizara ya afya inasema itaruhusu tu dozi ambazo zina muda wa kuhudumu wa kati ya miezi minne pekee kuingia nchini. Kenya inalenga kuwachanja watu milioni 19 kufikia mwezi Juni mwaka huu, ikiwa sasa imewafikia watu milioni 17.5.