1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kituo ambako mlipuko uliwaua 3, kilinyimwa kibali mara tatu

2 Februari 2024

Msemaji wa serikali ya Kenya Isaac Mwaura amesema rushwa na ukosefu wa ufuatiliaji wa taratibu za vituo vya gesi vinalaumiwa kuchangia mlipuko uliosababisha vifo vya watu 3 na kuwajeruhi watu 280 mjini Nairobi.

https://p.dw.com/p/4bygE
Wazima moto wakipambana na moto uliotokea baada ya mlipuko huo jijini Nairobi Februari 02, 2024..
Wazima moto wakipambana na moto uliotokea baada ya mlipuko huo jijini Nairobi Februari 02, 2024..Picha: Luis Tato/AFP

Alipozuru eneo la mkasa, msemaji wa serikali Isaac Mwaura alisema kituo cha kujaza gesi ambapo mlipuko huo ulitokea, kinahudumu kinyume cha sheria na kwamba kampuni husika inapaswa kuwafidia waathiriwa.

Soma: Mlipuko wa gesi jijini Nairobi waua watu watatu na kuwajeruhi 270

"Naam, ni bahati mbaya sana. Kama uonavyo hapa, hii ni yadi, yadi isiyo halali ya kujaza gesi, ambayo haikuwa imepewa leseni na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli, EPRA. Lakini basi waliendelea kufanya kazi katika eneo kama hilo la makazi, eneo lenye msongamano mkubwa, na inasikitisha sana kwamba imetokea. Inaonyesha tu jinsi, wakati mwingine tuna taasisi dhaifu, unajua, taasisi za utekelezaji, na bila shaka, kipengele cha rushwa ambacho kimesababisha vifo vya watu Wakenya wenzetu watatu," amesema Mwaura.

EPRA haikukubali maombi ya kituo kupewa kibali

Mamlaka inayodhibiti nishati na petroli Kenya EPRA, pia imesema ilikataa mara tatu maombi ya kampuni hiyo kupewa kibali cha kuweka kituo chake cha kuhifadhi na kujaza gesi katika eneo hilo ambapo mlipuko ulitokea kwa sababu, ni sehemu yenye wakaazi wengi.

Miongoni mwa maafa yaliyoshuhudiwa ni pia kuteketea kwa bohari, makaazi yaliyo karibu na vilevile magari eneo hilo la Embakasi Nairobi.
Miongoni mwa maafa yaliyoshuhudiwa ni pia kuteketea kwa bohari, makaazi yaliyo karibu na vilevile magari eneo hilo la Embakasi Nairobi.Picha: Luis Tato/AFP

Wakaazi walisema kwa muda mrefu wamekuwa wakihofia maafa hayo yatatokea, kwani wamekuwa wakiona malori ya gesi yakifika kila siku katika eneo hilo.

Douglas Kanja, Naibu Inspekta wa Polisi, amesema mlinzi katika eneo ulikotokea mlipuko tayari amekamatwa.

Ameongeza kuwa uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha mlipuko huo, ambao ripoti za vyombo vya habari nchini humo zimesema uliweza kusikika kilomita kadhaa kutoka hapo.

Kulingana na maafisa na watoa huduma za dharura, moto uliharibu bohari ya nguo iliyokuwa karibu, magari na makaazi kadhaa ya watu.

Soma pia: Moto wasababisha mauti Nairobi

Mnamo mwaka wa 2011, zaidi ya watu 100 waliuawa katika kitongoji duni cha eneo la Embakasi wakati mafuta yalipovuja kutoka kwa bomba na kusababisha moto.

Wengi wa wahasiriwa walichomwa kiasi cha kutotambulika.

Mnamo mwaka 2018, moto katika soko la Gikomba Nairobi uliua watu 15 wakiwemo watoto wanne na kujeruhi takriban 70.

Vyanzo: AFPE, RTRTV