Kavelashvili achaguliwa kuwa rais wa Georgia
14 Desemba 2024Matangazo
Kavelashvili ameshinda baada ya kupata kura 224 kati ya 300 kutoka kwa wajumbe wa jopo maalum la uchaguzi linalomchagua rais, linalodhibitiwa na chama tawala cha Georgian Dream, na ambalo limesusiwa na upinzani. Mwenyekiti wa Tume Kuu ya Uchaguzi, Giorgi Kalandarishvili, amesema Kavelashvili amechaguliwa kuiongoza Georgia kwa kipindi cha miaka mitano. Rais wa sasa Salome Zurabishvili ameutangaza uchaguzi huo kuwa ''batili'' na amekataa kujiuzulu. Waziri Mkuu wa Georgia, Irakli Kobakhidze amesema kuchaguliwa kwa Kavelashvili, kutatoa mchango mkubwa katika kuimarisha serikali ya Georgia, na uhuru wake, pamoja na kupunguza misimamo mikali na kile kinachojulikana kama migawanyiko.