1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel akutana na viongozi 12 wa Afrika mjini Berlin

30 Oktoba 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameahidi kuongeza hatua za serikali yake katika kusaidia sekta binafsi barani Afrika dhidi ya misukosuko ya kisiasa na utaratibu wa malipo usio wa kawaida.

https://p.dw.com/p/37OWY
Deutschland Afrika-Gipfel bei Bundeskanzlerin Angela Merkel
Picha: Reuters/A. Schmidt

Kansela Angela Merkel ametoa ahadi hiyo katika mkutano wa kilele mjini Berlin Ujerumani unaonuiwa kuongeza uwekezaji binafsi barani Afrika. 

Merkel amesema fedha za maendeleo zitakazotolewa zinapaswa kusaidia uwekezaji wa makampuni madogo na kiwango cha kati ya barani Ulaya na Afrika kupitia hisa na mikopo.

Deutschland Afrika-Gipfel bei Bundeskanzlerin Angela Merkel
Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

"Tunataka kutoa ishara bayana, tunapendelea ushirikiano mwema na wenyewe faida wa ujirani mwema kati ya afrika na ulaya ufanikiwe, sisi ni majirani, washirika na sisi wa ulaya tunamasilahi makubwa zaidi, kuona afrika yenye nguvu na matumaini mema ya kiuchumi na ili hilo kulifikia panahitajika sio tu vitega uchumi vya serikali bali zaidi kuliko vyote vya kibinafsi," alisema Merkel alipowahutubia wafanyabiahara na viongozi 12 wa Afrika waliohudhuria mkutano huo. 

Lengo hasaa la mkutano huu wa kilele ni kutoa nafasi nzuri za ajira kwa waafrika, kupunguza umasikini ambao pamoja na misukosuko ya kisiasa na vurugu ndio mambo yanayopelekea idadi kubwa ya waafrika kukimbilia barani Ulaya.

Viongozi 12 wahudhuria mkutano wa kilele wa Berlin Ujerumani

Merkel anahitaji uhusiano huu na mataifa ya Afrika kuonesha hatua iliyopigwa katika miaka yake 13 madarakani na hasa hatua yake ya mwaka 2015 ya kufungua milango ya Ujerumani kwa zaidi ya wahamiaji milioni moja. hapo jana Kansela huyo wa Ujerumani alitangaza kustaafu katika siasa ifikapo mwaka 2021.

Deutschland Afrika-Gipfel bei Bundeskanzlerin Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Afrika Kusini Cyril RamaphosaPicha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Mkutano huo wa uekezaji uliohudhuriwa na marais 12 akiwemo rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa,  Waziri Mkuu wa Ethiopia  Abiy Ahmed na rais wa Rwanda Paul Kagame, unanuiwa kuonesha bara la Afrika ni bara thabiti  kwa Ujerumani kuekeza.

Kansela wa Austria Sebastian Kurz anaeshikilia urais wa kupokezana katika Umoja wa Ulaya pia alihudhuria mkutano huo. Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sissi pia amehudhuria na anatarajiwa kukutana na Kansela Angela Merkel kwa mazungumzo. Mkurugenzi mkuu wa shirika la fedha duniani IMF Christine Lagarde pia amehudhuria pamoja na maafisa kadhaa wa maendeleo ya kimataifa.

Muandishi Amina Abubakar/dpa/Reuters 

Mhariri: Yusuf Saumu