1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huawei inataka mahakama kuibatilisha sheria hiyo.

7 Machi 2019

Kampuni kubwa ya kutengeza simu ya China, Huawei imeishtaki serikali ya Marekani ikipinga sheria iliyopitisha mwaka jana inayokataza taasisi za serikali za Marekani kununua bidhaa za Huawei

https://p.dw.com/p/3Eapt
China Huawei Vorsitzender Guo Ping
Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Cheung

Mwenyekiti wa Huawei Guo Ping amesema kwamba wamelazimika kwenda mahakamani kwa sababu Marekani imeshindwa mara kadhaa kutoa uthibitisho wa kuonyesha haja ya kuweka marufuku hiyo ambayo inaweza kuwatoa katika ushindani wa kibiashara wa kutoa huduma ya kasi ya mtandao wa 5G.

Kesi hiyo iliyowasilishwa katika mahakama moja katika jimbo la Texas inakipinga kipengee cha 889 katika kifungu cha sheria za mamlaka ya usalama wa taifa wa Marekani iliyotiwa saini mwezi Agosti mwaka jana na rais wa Marekani Donald Trump.

Huawei 2019 CES in Las Vegas
Wateja wakishiriki katika maonyesho ya bidhaa za Huawei Las Vegas, Nevada, MarekaniPicha: Reuters/S. Marcus

Sheria hiyo imezikataza taasisi za serikali ya Marekani pamoja na wakandarasi wake kununua vifaa au huduma za kampuni ya Huawei.

Guo anasema katika kesi hiyo pia watadai fidia kutokana na hasara mbali mbali zinazojiri kutokana na sheria hiyo.

Akizungumza na wanahabari katika makao makuu ya kampuni hiyo katika mji wa Shenzhen, Kusini mwa China, Guo amesema Marekani inatumia kila mbinu kuipaka tope kampuni ya Huawei akiongeza kwamba Marekani imedukua mitambo mikuu ya kampuni hiyo na kuiba barua pepe na vyanzo vya kodi zao.

Marekani imekuwa na hofu ya usalama juu ya vifaa vya Huawei 

Kwa muda sasa Marekani imekuwa ikiamini kwamba kampuni ya Huawei ni tishio kwa usalama wake hasa kwa kuzingatia tajriba ya mwanzilishi wa kampuni hiyo Ren Zhengfei aliyekuwa muhandisi wa jeshi la China.

Symbolbild Huawei
Simu ya mkononi ikiwa na nembo ya HuaweiPicha: picture-alliance/NurPhoto/J. Arriens

Hofu ya Marekani imezidi baada ya kampuni hiyo kupanuka zaidi kote Ulimwenguni na kuongoza katika vifaa vya mawasiliano vinavyounganisha sehemu kubwa ya mataifa ulimwenguni na vile vile Huawei ni mojawapo ya kampuni kubwa zinazotengeneza simu za kisasa.

Marekani imeonya kwamba vifaa vya Huawei vinaweza kutumiwa na serikali ya China kuyapeleleza mataifa mengine na kuharibu mawasiliano muhimu hivyo basi kuyataka mataifa kuisusia kampuni hiyo.

Upande wake Huawei inaeleza kwamba kampuni hiyo iliyo na matawi katika nchi 170 haijawahi kushiriki katika uvunjaji wa sheria zozote za kiusalama na pia haijwahi kupokea maombi kutoka kwa serikali ya China kuweka vifaa vya siri kuiwezesha kufanya ujasusi.

Mwandishi: Faiz Musa/RTRE/AFPE

Mhariri: Iddi Ssessanga