1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yaonya huenda virusi vya corona visikabiliwe vilivyo

14 Mei 2020

Kampuni ya dawa ya Sanofi imehakikisha kuwa itatoa chanjo ya corona kwa mataifa yote itakapokuwa tayari huku mamlaka ya dawa ya Umoja wa Ulaya ikidokeza kwamba chanjo hiyo huenda ikawa tayari katika muda wa mwaka mmoja.

https://p.dw.com/p/3cED6
Symbolbild | Forschung | Impfstoff | Covid-19
Picha: picture-alliance/Zoonar

Matamshi ya mkurugenzi mkuu wa kampuni ya kutengeza madawa ya Sanofi Paul Hudsons, yameibua hisia kali kutoka kwa serikali ya Ufaransa. Kupitia kituo cha redio cha Sud, naibu waziri wa uchumi Agnes Pannier- Runacherwa amesema kuwa haitakubalika kwamba taifa jengine linapewa kipaombele cha kupata chanjo hiyo kwa kisingizio cha sababu za kifedha.

Katika taarifa iliyotolewa leo, kampuni hiyo ya Sanofi imesema kuwa imekuwa ikijitahidi katika hali zisizo za kawaida kutoa chanjo yakekwa wote na kwamba ushirikiano wake na taasisi ya utafiti na maendeleo ya dawa za kibayologia  ya Marekani BARDA, unairuhusu kuanza utengenezaji wa chanjo hiyo mapema iwezekanavyo.Rais wa kampuni hiyo nchini Ufaransa Olivier Bogillot, ameliamba shirika la habari la Ufaransa la France Info kwamba Marekani inaharakisha mahitaji ya kisheria kutengeneza chanjo na kwamba bara Ulaya pia linapaswa kuchukuwa hatua kama hiyo.

USA Sanofi Paul Hudson
Paul Hudson- Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya SanofiPicha: Imago Images/IP3press/C. Morin

Wakati huo huo, mkurugenzi wa shirika la afya duniani WHO katika kanda ya Ulaya Dkt Hans P. Kluge amesema kuwa mienendo ya watu ndio itakayotoa mwelekeo kuhusu janga la virusi vya corona. Kluge amesema kuwa huku serikali zikianza kuondoa vikwazo, ni jukumu la kibinafsi na pia la pamoja na kutoa wito kwa watu kufuata mapendekezo ya serikali zao ya kupunguza kukaribiana, kuendelea kunawa mikono na kupunguza hatari kwa makundi dhaifu katika jamii kama vile wazee na wagonjwa wanaotegemea maamuzi yanayofanywa na watu.   

Huku hayo yakijiri, viongozi wa dunia wa sasa na waliopita wamesisitiza kwamba chanjo yoyote ya baadaye pamoja na tiba zinapaswa kufikia kila moja bila malipo huku idadi ya waliofariki kutokana na ugonjwa wa COVID-19 ikifikia watu elfu 300 kote duniani. Janga la virusi vya corona limesababisha mporomoko katika sekta za kijamii na kiuchumi kote duniani na wakati baadhi ya mataifa yakianza kulegeza vikwazo vyake, hofu ya wimbi la pili la maambukizi imesababisha biashara nyingi kufungwa na watu kubakia majumbani.

Lakini shirika la afya duniani, limeonya jana kuwa huenda virusi hivyo visikabiliwe vilivyo. Michael Ryan, mkurugenzi wa hali za dharura katika shirika hilo la WHO, amesema kuwa huenda virusi hivyo vikawa kama janga lingine katika jamii zetu kama vile ugonjwa wa Ukimwi ambao haujamalizika lakini watu wamejifunza kuishi nao.