1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampuni sita za Kichina za madini zafungiwa Congo

23 Agosti 2021

Mamlaka katika mkoa wa Kivu Kusini nchini Congo zimesimamisha shughuli za kampuni sita za china za uchimbaji madini katika wilaya ya Mwenga ili kuhifadhi maslahi ya wakaazi wa vijiji kunakochimbwa dhahabu

https://p.dw.com/p/3zN9D
Neues Bergbaugesetz in der RD Kongo
Picha: Getty Images/AFP/S. Tounsi

Hatua hiyo iliyochukuliwa na gavana wa mkoa wa Kivu kusini Théo Ngwabidje Kasi mwishoni mwa juma inahusu eneo la Mwenga lililoko umbali wa karibu kilomita 100 kusini magharibi mwa mji wa Bukavu ambapo kunafanyika shughuli nyingi za uchimbaji wa dhahabu.

Katika agizo lake, gavana wa mkoa wa Kivu Kusini amesisitiza kuwa ni muhimu kuweka utaratibu na pia kurejesha utulivu katika sekta ya uchimbaji wa madini wa viwandani katika eneo hilo lenye uhasama wa mara kwa mara kati ya wakaazi na wachimba-dhahabu raia wa China na pia kulinda maslahi ya wakazi wa eneo hilo, na mazingira na haki za binadamu.

Kwa  muda mrefu, asasi mbalimbali za kiraia katika wilaya ya Mwenga zilitoa malalamiko na kukosoa kampuni hizo za kichina kuchimba dhahabu kwa siri bila kuwa na hati rasmi zinazowapa kibali, zingine zikilindiwa usalama na askari wa jeshi la Congo FARDC walioonekana katika migodi ya uchimbaji madini, kuchimba dhahabu bila kwanza kufanya utafiti wa athari za kimazingira kama inavyotakiwa na sheria ya madini inayotumika nchini DRC; matumizi ya kemikali ambazo zinaingia  kwenye mito ya Elila na Zalya zikiwa na athari kwa afya ya binadamu, shughuli zinazofanywa bila hata ya kuwashirikisha wakaazi wa eneo hilo. Christian Wanduma ni mshauri kisheria wa kitongoji cha Wamuzimu katika wilaya ya Mwenga:

Awali, gavana Ngwabidje alitoa tangazo la kuamuru askari waondoke kutoka migodi hiyo, na baadae kuchukua amri hiyo mpya inayowataka wafanyikazi wote raia wa kigeni na wa Congo wanaotumikia kampuni hizo pamoja na washirika wao waondoke mara moja kwenye maeneo ya madini, na kuwa vifaa vyao vya kufanya kazi vitabaki hapo hadi iundwe kamati ya muda itakayofanya uchunguzi kesi moja baada ya nyingine na kutoa mwangaza zaidi. Mamlaka ya kivu kusini inalenga pia kusambaaza hatua hii katika maeneo mengine kama vile Shabunda, Fizi na Kalehe.

Mitima Delachance, DW, Bukavu