1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamati ya Marekani inayohusika na wakimbizi yatoa ripoti yake kwa 2004.

Mohammed AbdulRahman25 Mei 2004

Inasema mkataba wa 1951 kuhusu haki za wakimbizi unaendelea kuvunjwa.

https://p.dw.com/p/CHij
Watoto wakimbizi wa Sudan walioingia nchi jirani ya Chad.
Watoto wakimbizi wa Sudan walioingia nchi jirani ya Chad.Picha: AP

Kwa mujibu wa ripoti ya makadirio ya wakimbizi duniani ya 2004 iliotolewa na Kamati ya Marekani inayohusika na wakimbizi (USCR) ni kwamba zaidi ya wakimbizi milioni 7 katika jumla ya karibu milioni 12 duniani wamewekwa katika makambi kwenye maeneo ya hatari ya mipakani au katika sehemu za madongo poromoka mijini, bila ya kutaluiwa maanani haki za msingi za binaadamu. Wengi wao amekuweko katika hali hiyo kwa zaidi ya miaka 10

Ripoti hiyo iliogundua ongezeko kubwa mno la idadi ya watu waliotawanyika ndani ya nchi zao-watu waliolazimishwa kuyahama makaazi yao lakini wakiwa bado katika nchi zao- katika kipindi cha mwaka jana 2003, ni kwamba kuwaweka watu katika makambi kwa muda mrefu ni kitu ambacho hakihalaliki kabisa kisheria na pia katika mtazamo wa kiutu hakikubaliki kabisa.

Utaratibu huo ni wa kuwaweka wakimbizi katika hali inayofanana na kizuizi na kuwawekea mipaka katika utaratibu wao wa kimaisha-ikiwa ni kwenda kinyume na haki za msingi za binaadamu chini ya mkataba wa wakimbizi wa 1951.

Kwa mujibu wa mhariri wa makala maalum katika ripoti ya mwaka huu ya kamati hiyo ya wakimbizi ya Marekani Merrill Smith, kutolewa hadharani kwa ripoti hiyo kunafungua milango ya kuanza kampeni duniani kote, kuzishinikiza serikali na jumuiya ya kimataifa zisitishe utaratibu huo wa kuwaweka wakimbizi makambini na kuwapa haki kamili kama inavyofafanuliwa katika mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbizi.

Ripoti ya mwaka huu imegundua kwamba idadi ya wakimbizi na wanaosaka hifadhi ya ukimbizi, ilipungua 2003, kutoka karibu milioni 13 mwishoni mwa 2002 hadi milioni 11.9 mwanzoni mwa mwaka huu 2004. Kupungua huko, zaidi kunatokana na kurudi nyumbani kwa karibu wakimbizi 613,000 wa Kiafghan waliokuweko Iran na Pakistan na kurudi kwa karibu wakimbizi 130,000 nchini Angola, baada ya vita vya miaka 27 vya wenyewe kwa wenyewe.

Lakini wakati idadi ya kupungua wakimbizi likiwa jambo la kutia moyo, hata hivyo wakimbizi waliolazimika kutawanyika ndani ya nchi zao wakiyahama makaazi yao, iliongezeka kutoka kiasi ya milioni 22 mwanzoni mwa 2003 hadi milioni 23.6 mwishoni mwa mwaka huo uliopita.

Ongezeko kubwa zaidi ni katika mataifa ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara hasa nchini Sudan, ambako zaidi ya watu milioni moja wenye asili ya kiafrika walilazimishwa kuyahama maskani yao katika mkoa wa magharibi wa Darfur, kutokana na mashambulio na hujuma za pamoja za majeshi ya serikali na wanamgambo wa kiarabu wanaojulikana kama Janjawid. Kiasi ya wakaazi wengine 120,000 wa Darfur wakalazimika kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani ya Chad.

Kwa kuwa wakimbizi wanakimbilia maeneo mengine ndani ya nchi zao ni shida kuwagundua-ripoti ya kamati ya Marekani inayohusika na suala la wakimbizi duniani inaema, idadi kamili ya waliokubwa na janga la aina hiyo katika kila nchi haijulikani- ama makadirio yanaonyesha huenda ikawa kubwa kuliko inavyofikiriwa.

Ripoti hiyo inasema huko Sudan pekee, kukiwa na kiasi ya watu milioni 4.8 waliotawanyika ndani nchini- hiyo ni takriban 20 asili mia ya watu waliokumbwa na janga kama hilo duniani kote. Inafuatiwa na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo inayokadiriwa kuwa na watu milioni 3.2 waliotawanyika, Colombia karibu milioni 3 na Uganda kiasi ya milioni 1.4.

Nchi sita za kiafrika-Sudan , Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Uganda, Angola, Ivory Coast na Liberia kwa pamoja zina jumla ya watu nusu milioni waliolazimika kuyahama makaazi yao na kutawanyika katika nchi hizo, hadi mwishoni mwa mwaka jana.

Wakati maelfu ya Waafghan wakiwa wamerejea nyumbani baada ya kuangushwa utawala wa Taliban mwishoni mwa 2001, idadi kubwa ya wakimbizi duniani hadi mwisho wa 2003, ilikua ni Palestina-kiasi ya milioni tatu, wakitawanyika katika ukanda wa Gaza, Ukingo wa magharibi hadi Syria, Lebanon na sehemu nyengine za Mashariki ya kati- 37 asilia mia ya idadi jumla ya wakimbizi duniani. ikifuatwa na bara la Afrika –kiasi ya wakimbizi 3.2 kwa jumla wakiwa ni 27 asili mia Inafuatiwa na eneo la kati na kusini mwa Asia kwa jumla ya wakimbizi 1.9 milioni, wengi wakiwa Wafghan wanaoishi Pakistan. Kwa jumla wengi wa wakimbizi hao wanaishi katika makambi katika hali ambazo ni kinyume na ufafanuzi wa mkataba wa 1951 unaozitaka nchi husika kuwapatia wakimbizi nafasi ya kufanya kazi, kutembea bila vipingamizi, kuwa na haki ya kumiliki mali na kupata elimu-yakiwa ni miongoni mwa haki zao za msingi kuwawezesha kuishi maisha ya kawaida na ya kiutu.

Kwa mfano ripoti hiyo inataja juu ya zaidi ya wakimbizi nusu milioni kutoka Myanmaar(Burma) ambao wamekua wakiishi bila ya kuwa na haki ya kufanya kazi au kusafiri kwa zaidi ya miaka 20 katika nchi za Thailand, Bagladesh, Malaysia na India. Na huko Sudan watu nusu milioni wamekwama katika makambi au maeneo maalum katika misingi ya kibaguzi ilioendelea kwa miongo miwili. Chini ya zingatio la yote hayo, ripoti ya 2004 kuhusu janga la wakimbizi waliotawanyika ndani ya nchi zao, ya kamati inayoshughulikia wakimbizi ya Marekani-USCR- inasisitiza kwamba mkataba wa kimataifa kuhusu hifadhi na haki ya wakimbizi hauna budi kuheshimiwa.