1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kagame: Mazungumzo ya usalama wa Rwanda na Burundi yaendelea

Sylivanus Karemera21 Desemba 2020

Rais Paul Kagame wa Rwanda amesema mazungumzo yanafanyika baina ya nchi yake na  Burundi kuhusu usalama kati ya nchi hizo majirani. Kagame ameyasema hayo katika hotuba yake kuhusu hali ya nchi.  

https://p.dw.com/p/3n11w
Ruanda vor den Wahlen 2017
Picha: Imago/Zumapress/M. Brochstein

Rais Paul Kagame alikuwa akizungumza mubashara kupitia runinga ya taifa akiwa Ikulu mjini Kigali. Waandishi wa habari walikuwa kwenye ukumbi mwingine wa Kigali conference Center ambapo badaye walipewa nafasi ya kuuliza maswali kuhusu masuala mbalimbali.

Pamoja na mambo mengine Rais Paul Kagame amezungumzia usalama katika mpaka hususan juu ya kinachoendelea baina ya Rwanda na mataifa ambayo kwa miaka ya hivi karibuni yamekuwa na matatizo na nchi yake. Amesema kwa sehemu kubwa hali ni shwari, akionya lakini juu ya mapungufu katika baadhi ya maeneo.

"Tatizo kidogo tulilo nalo liko upande wa Kusini kwenye mpaka na majirani zetu, ndugu zetu na jirani zetu wa Burundi, kuna mazungumzo yanayoendelea baina yetu ili kutafuta juhudi za jinsi gani usalama wetu usiendelee kuharibika hasa kuanzia kwa majirani zetu. Upande wa magharibi kunakopatikana nchi ya DRC wao ushirikiano wetu ulianza mapema tangu kulipopatikana mabadiliko ya utawala, naweza kusema kwamba matatizo yaliyokuwepo yanaendelea kupungua kabisa." Amesema Kagame.

Kagame asema hatua zimepigwa katika kupunguza msuguano na Uganda
Kagame asema hatua zimepigwa katika kupunguza msuguano na UgandaPicha: Getty Images/AFP/M. Sibiloni

Lakini alipokuwa akizungumzia upande wa kaskazini katika mpaka wa Rwanda na Uganda nchi ambayo kimsingi imekuwa na matatizo na Rwanda amesema kuwa hali ijapokuwa haijatengamaa lakini kuna hatua iliyopigwa.

Kuanzia jana jumapili Rwanda ilituma idadi isiyojulikana ya wanajeshi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati siku nne kabla ya nchi hiyo kuingia kwenye uchaguzi mkuu wa Rais. Jeshi la Rwanda lilithibitisha kuondoka kwa kikosi hicho ambacho ilisemekana kinakwenda kuongeza nguvu kwa majeshi ya Rwanda yaliyopo tayari nchini humo ili kulinda usalama wakati wa uchaguzi pamoja na kupambana na wapiganaji wanaongozwa na Rais wa zamani wa nchi hiyo Francois Bozize.

Rais Kagame akasema "Hivi karibuni kulikuwa na mashambulizi ya makundi yaliyotokea mahali fulani kutoka nje ya Jamhuri ya kati lakini likiendeshwa na wana-Jamhuri ya kati, wakaanza kujikusanya pamoja na baadaye nikaambiwa baadhi ya makundi yanamtii Rais wa zamani wa nchi hiyo Francois Bozize, naambiwa lengo lao lilikuwa ni kuharibu uchaguzi mkuu lakini kikubwa zaidi kwetu ni kwamba walishambulia wanajeshi wetu."

Rwanda yatumia drones kupambana na corona

Ama kuhusu ugonjwa COVID-19, Rais Kagame amesema Rwanda tayari imeshaweka mikakati mikali kuhusu kupambana na wimbi jipya la maambukizi ya ugonjwa huo ambapo kuanzia siku ya Jumanne tarehe 22 mwezi huu hakuna mtu atakeruhusiwa kutembea baada ya saa mbili za usiku.Rais Kagame amesema kwamba haya yote yanafanyika katika juhudi za kuhakikisha kwamba wanawalinda wananchi dhidi ya janga hili.

"Tumefikia mahali ambapo haaytuwezi kukubali kwamba juhudi zote tulizoziweka kujilinda dhidi ya janga kupotea bure, huu si wakati wa kubweteka isipokuwakuhakikisha mafanikio yetu hayaharibiki." Ni kauli yake Kagame

Zaidi ya watu elfu saba na mia saba ndiyo wamekwishaathirika na ugonjwa Corona nchini Rwanda, huku wengine wapatao elfu sita wakipona na tayari watu 63 wakishapoteza maisha yao.

Mwandishi: Sylivanus Karemera/DW Kigali

Mhariri: Daniel Gakuba