1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kagame atetea rekodi ya Rwanda kuhusu demokrasia

Sylvia Mwehozi
22 Juni 2024

Rais wa Rwanda Paul Kagame ametetea hali ya kidemokrasia katika taifa hilo wakati akifungua kampeni za uchaguzi wa rais wa Julai 15 zilizoanza rasmi Jumamosi

https://p.dw.com/p/4hOGd
Rais wa Rwanda Paul Kagame
Rais wa Rwanda Paul Kagame Picha: Jean Bizimana/REUTERS

Rais wa Rwanda Paul Kagame ametetea hali ya kidemokrasia katika taifa hilo wakati akifungua kampeni za uchaguzi wa raiswa Julai 15 zilizoanza rasmi siku ya Jumamosi. Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliohudhuriwa na maelfu ya wafuasi, wengi wao wakiwa wamesafirishwa kwa mabasi kufika katika uwanja wa kampeni, Kagame ametetea rekodi ya Rwanda kuhusu demokrasia na kuwanyoshea kidole wakosoaji wake juu ya madai ya kukandamiza wapinzani.

Kiongozi huyo ameueleza umati wa wafuasi kuwa mara nyingi watu wanatofautiana ama kuelewa tofauti lakini kwake yeye demokrasia inamaanisha kuchagua kile kilicho bora na mtu anachokitaka. 

Takribani Wanyarwanda milioni 9 wameandikishwa kushiriki uchaguzi huo wa urais ambao kwa mara ya kwanza utafanyika sambamba na ule wa bunge. Rais Kagame anachuana na wapinzani wawiliambao pia waliwania nafasi hiyo katika uchaguzi uliopita wa 2017.