1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kadinali Pell apatikana na hatia ya uhalifu wa kingono

26 Februari 2019

Kadinali wa Australia George Pell, mmoja wa washauri wa karibu sana wa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis, amepatikana na hatia ya kuwanyanyasa kingono wavulana wawili

https://p.dw.com/p/3E6PJ
Australien Kardinal George Pell
Picha: Getty Images/D. Traynor

Baraza la waamuzi mahakamani nchini Australia mnamo mwezi Desemba kwa kauli moja lilimkuta Pell na hatia ya mashitaka matano ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya wavulana wawili katika Kanisa la Mtakatifu Patrick's mjini Melbourne katika miaka ya 1990.

Pell, waziri wa zamani wa uchumi wa Vatican ambaye sasa ana umri wa miaka 77, anatuhumiwa kwa kuwapeleka wavulana hao – wakati huo wakiwa na umri wa miaka 12 na 13 – katika chumba cha kuhifadhi vitu vya thamani na nyaraka za kanisa baada ya misa ya Jumapili na kuwalazimisha kufanya naye kitendo cha ngono 

Mhubiri huyo ambaye muda amekuwa huru kwa dhamana, alikanusha mashitaka yote na kesi ya awali ikakamilika kwa majaji kutofikia uamuzi mnamo Septemba, lakini akashitakiwa upya Desemba 11.

Amri ya mahakama iliyotolewa na jaji aliyeongoza kesi hiyo ilivizuia vyombo vya habari kuripoti kuhusu kesi hiyo pamoja na vikao vilivyofuata tangu Mei. Amri hiyo iliondolewa wakati wa kikao cha mahakama leo baada ya kanzishwa kesi ya madai mengine tofauti dhidi ya Kadinali huyo ya vitendo vilivyofanywa katika miaka ya 1970.

Hakujawa na kauli yoyote kutoka makao makuu ya kanisa Katoliki mjini Vatican, lakini Pell alisisitiza leo kuwa hana hatia.

Taarifa iliyotolewa na mawakili wa wake imesema kuwa wamekata rufaa kupinga hukumu hiyo. Wamesema madai mengi na mashitaka mengine dhidi ya Pell tayari yalikuwa yamefutwa.

Mmoja wa wavulana hao wawili waliokuwa wakiimba kwaya ambao Pell alipatikana na hatia ya kuwanyanyasa, alifariki dunia mwaka wa 2014 baada ya kutumia dawa za kulevya kupindukia, kifo ambacho familia yake ilisema ni kutokana na maumivu ya kiakili kutokana na alichokipitia.

Pell anatarajiwa kubaki kizuizini akisubiri kujua hatima yake. Waendesha mashitaka wanasema anakibiliwa na hadi miaka 25 jela kama kesi yake ya rufaa itakataliwa.

Habari za hukumu yake ni pigo kubwa kwa kanisa Katoliki ambalo linapata changamoto ya kuushawishi ulimwengu kuwa imelivalia njuga suala la unyanyasaji wa watoto kingono. Siku mbili zilizopita, Papa Francis aliufunga mkutano wa kilele wa kihistoria mjini Vatican kuhusu unyanyasaji wa kingono unaofanywa na makasisi

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Caro Robi