1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya Kiarabu yaruhusu waangalizi wake kubakia Syria

Mohammed Khelef9 Januari 2012

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Kiarabu wameamua kuiruhusu timu ya waangalizi wa Jumuiya hiyo, kukamilisha kazi yao ya mwezi mmoja nchini Syria, licha ya lawama kali zinazotolewa kwa waangalizi hao.

https://p.dw.com/p/13gFB
Wajumbe wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wakikutana mjini Cairo, Misri.
Wajumbe wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wakikutana mjini Cairo, Misri.Picha: Reuters

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana baada ya mawaziri hao kumaliza mkutano wao mjini Cairo, Misri, kwa sasa Jumuiya ya Kiarabu haitaomba uingiliaji kati wa Umoja wa Mataifa. Taarifa hiyo pia imeitaka serikali ya Syria na makundi yote yenye silaha, kuacha mara moja vitendo vya vurugu.

Mkutano huo umefanyika katika wiki ya pili ya waangalizi wa Jumuiya ya Kiarabu kuingia nchini Syria, kuangalia ikiwa serikali ya Rais Bashar al-Assad, inatekeleza masharti ya mpango wa amani ulioandaliwa na Jumuiya hiyo. Ujumbe wa waangalizi hao, umelaumiwa kwa kushindwa kuzuia ukandamizaji wa vikosi vya serikali dhidi ya raia.

Wakati huo huo, mauaji yameendelea nchini Syria, huku watu 40 wakiuawa mwishoni mwa wiki. Taarifa hizo zimetolewa na makundi ya haki za binaadamu, lakini imekuwa shida kuzithibitisha kwa kuwa serikali imezuia waandishi wa habari wa kigeni, kuingia nchini humo. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu 5,000 wameshauwa hadi sasa, tangu maandamano dhidi ya utawala wa Assad yaanze mwezi Machi mwaka jana.