1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kuwapokonya silaha wanamgambo wa DRC

11 Machi 2022

Mratibu wa mpango wa kuwanyang'anya silaha wapiganaji wa zamani na kuwarejesha kwenye maisha ya kawaida katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Tommy Tambwe, amekutana na wawakilishi wa makundi yenye silaha.

https://p.dw.com/p/48LBk
DR Kongo 2003 | Milizen
Picha: Stephen Morrison/dpa/picture alliance

Majadiliano hayo yaliyofanyika mjini Uvira, yanawajumuisha wawakilishi wa makundi yenye silaha yanayokadiriwa kuwa zaidi ya 40, waliotoka katika vijiji kadhaa za wilaya za Uvira, Fizi na Mwenga

Makundi hayo yamekuwa yakipambana kati yao kwa malengo ya kikabila na kujaribu kumiliki ardhi na migodi yenye madini upande mmoja, na upande mwingine yanapambana dhidi ya ngome za jeshi la Kongo FARDC kwa malengo ya kujipatia silaha.

Wakati wa majadiliano hayo, Tambwe mratibu wa mpango wa kuwanyang'anya silaha unaofahamika kwa kifupi kama PDDRC-S amesisitiza kwamba majadiliano hayo hayajatoa bahati au fursa kwa wanamgambo hao kutoa masharti ya mahitaji yao kwa serikali, ila ni muda mwafaka kwake kuhamasisha wanamgambo kuweka silaha chini kwa hiari, kukagua mapendekezo ya mijadala ya tangu awali na kwa nini haijatekelezwa, na baadae kwa pamoja kuchukua mikakati maalum itakayosababisha amani ya kudumu, kama inavyotakiwa na serikali. 

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Congo, MONUSCO kimeahidi kuziunga mkono hatua zote za harakati ya kuwanyang'anya silaha wanamgambo mashariki ya Congo. Kiongozi wa ofisi ya MONUSCO mkoani Kivu Kusini, Karna Soro anawaonya wanamgambo hao.

Jeshi la DR Congo layashambulia makundi yenye silaha Kigoma

''Nadhani mazingira wezeshi yapo sasa, mpango wa serikali upo, washirika wa mpango huo pia wamehamasishwa... Hivyo sasa, kwa ajili ya jamii zetu na nchi yetu nzima, nadhani ni wakati wa kukomesha mateso haya,'' amesema Karna. 

Wawakilishi wa makundi hayo ya wanamgambo pia wameikosoa serikali ya Kongo kushindwa kuwahudumia wapiganaji wa zamani waliofuata wito wake wa kuweka silaha chini, huku wengi wa waliojisalimisha hapo awali, wameamua tena kurejea msituni kutokana na maisha magumu waliopitia baadae.