1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Johnson ajiondoa kinyang'anyiro cha uwaziri mkuu Uingereza

24 Oktoba 2022

Waziri Mkuu wa zamani Boris Johnson amejiondoa kwenye kinyang'anyiro cha uwaziri mkuu. Hatua hiyo imemuacha Rishi Sunak akipigiwa upatu kuchaguliwa kwenye wadhifa huo.

https://p.dw.com/p/4IaL3
Großbritannien Ex-Premier Boris Johnson
Picha: Gareth Fuller/PA via AP/picture alliance

Wiki chache tu baada ya kushindwa katika azma yake ya kukiongoza chama hicho, huenda sasa hali itabadilika kwa Sunak na kutangazwa mkuu wa chama hicho leo, hasa baada ya Boris Johnson aliyetizamwa kuwa mshindani wake mkuu kutangaza kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho usiku wa kuamkia leo

Kinyang'anyiro hicho kimetokana na aliyekuwa Waziri Mkuu Liz Truss kujiuzulu siku ya Alhamisi wiki iliyopita.

Mshindi anahitajika kuungwa mkono na wabunge wasiopungua 100 wa chama cha Conservative kwa njia ya kura. Shughuli hiyo ya kupiga kura imepangwa kufanyika leo mchana.

Conservative waanza mbio za kumsaka mrithi wa Truss

Mnamo Ijumaa usiku Sunak tayari alikuwa anaungwa mkono na takriban wabunge 150 wa chama hicho.

Penny Mordaunt, mshindani pekee wa Sunak

Rishi Sunak apigiwa upatu kuwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza
Rishi Sunak apigiwa upatu kuwa Waziri Mkuu mpya wa UingerezaPicha: Kirsty Wigglesworth/AP/dpa

Hatua ya Boris Johnson kutangaza kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho hata kabla atangaze rasmi kuwa angewania, imemuacha waziri Penny Mordaunt kuwa mshindani pekee wa Sunak.

Hata hivyo Mordaunt hajapata uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa wabunge wa chama chake.

Anatarajiwa kukabiliwa na shinikizo kubwa kuachana na azma hiyo ili kukamilisha shughuli ya kumpata waziri mkuu mpya mapema, mnamo wakati Uingereza ikikabiliwa na migogoro kadhaa.

Ikiwa Mordaunt mwenye umri wa miaka 49 atakataa kuachana na azma yake, na aweze kupata kura 100, basi uamuzi utafanywa na wanachama 170,000 wa Conservative kwa kupiga kura baadaye wiki hii mtandaoni na matokeo kutangazwa Ijumaa.

Miezi miwili iliyopita, wanachama walimchagua Truss aliyemshinda Sunak, licha kwamba Sunak alikuwa na uungwaji mkono wa wabunge wengi wa Conservative kuliko Truss.

Kinyang'anyiro kimebaki kati ya Penny Mordaunt na Rishi Sunak
Kinyang'anyiro kimebaki kati ya Penny Mordaunt na Rishi SunakPicha: Avalon/Photoshot/picture alliance

Wachambuzi wanasema Mordaunt ni maarufu miongoni mwa wanachama.

Hatua ya kwanza kwenye kinyang'anyiro hicho ni jumla ya wabunge 357 wa Conservative kupiga kura ya ishara alasiri ya leo kuonesha ni mgombea yupi anaungwa mkono zaidi katika chama hicho ambacho kwa sasa kimegawika.

Je chama cha Conservative kitampata Waziri Mkuu Mpya atakayeleta mshikamano?

Hii ni mara ya pili ndani ya miezi miwili kwa chama cha Conservative kumchagua waziri waziri mkuu mpya ndani ya miezi miwili.

Liz Truss aliyekuwa amehudumu kwa siku 44 pekee, alijiuzulu wiki iliyopita baada ya mpango wake wa punguzo la kodi kuzusha mtikisiko katika masoko ya fedha.

Truss afanya kikao chake cha kwanza na timu yake ya mawaziri

Truss alichukua usukani mapema mwezi Septemba kutoka kwake Boris Johnson ambaye pia alilazimika kujiuzulu kufuatia kashfa ya sherehe iliyoandaliwa wakati wa vikwazo vya kudhibiti virusi vya corona na vilevile kwa kulidanganya bunge kuhusu sherehe hiyo.

Wakosoaji wakuu ndani ya chama hicho walitahadharisha kwamba kungeshuhudiwa wimbi la wabunge wake kujiuzulu endapo Johnson angerejea tena kuwa waziri mkuu, hali ambayo ingesababisha uchaguzi mkuu unaoitishwa na vyama vya upinzani kuandaliwa.

Kinyang'anyiro cha kumrithi Boris Johnson mwezi Septemba kilikuwa kati ya Rishi Sunak na Liz Truss.
Kinyang'anyiro cha kumrithi Boris Johnson mwezi Septemba kilikuwa kati ya Rishi Sunak na Liz Truss.Picha: Paul Faith/AFP

Kwa sasa uchaguzi mkuu unapaswa kufanyika baada ya miaka miwili ijayo.

Baadhi ya waliowahi kumuunga mkono Boris Johnson kama waziri wa ndani Grant Shapps kwa sasa wanamuunga mkono Sunak.

Mnamo Jumamosi, Boris Johnson ambaye ni miongoni mwa wanasiasa walioongoza kampeni za Brexit, alikatisha likizo yakekatika kanda ya Karibea na kurudi jijini London, huku akiungwa mkono na mawaziri kadhaa akiwemo waziri wa mambo ya nje James Cleverly na wa Biashara Jacob Rees-Mogg kuwania uwaziri mkuu tena baada ya Truss.

Lakini katika ishara ya kudidimia kwa hadhi yake kisiasa, Johnson alijiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho akisema "huwezi ukatawala vyema, ikiwa huna chama ambacho kimeungana bungeni”.

Utafiti wa maoni uliofanywa mwishoni mwa wiki ulidokeza kuwa huenda chama cha Conservative kikanufaika kubadilisha kiongozi wao baada ya hatua za Truss kuwashusha chini kisiasa.

(AFPE)