1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JOHANNESBURG: Bunge la Afrika lapendekeza Zimbabwe ichunguzwe.

12 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CC31

Bunge la Afrika limepiga kura kuidhinisha uamuzi wa kupeleka ujumbe wa kuchunguza madai ya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Zimbabwe.

Wabunge mia moja arobaini na tisa waliunga mkono uamuzi huo ilhali wabunge ishirini na tisa waliupinga.

Wakati wa kujadili hoja hiyo, wabunge kadha waliushutumu utawala wa Rais Robert Mugabe kwa kutumia nguvu kukabiliana na wapinzani wake.

Bunge hilo halina uwezo wa kutoa uamuzi dhidi ya mataifa wanachama hasa ikizingatiwa kwamba mataifa ya bara la Afrika yamekuwa yakijiepusha kuzikosoa waziwazi sera za Rais Robert Mugabe.

Serikali ya Zimbabwe imesema huenda ujumbe huo usiruhusiwe kuingia nchini humo.

Waziri wa Habari Sikhanyiso Ndlovu aliwaambia waandishi wa habari mjini Harare kwamba Zimbabwe ni nchi huru wala haifai kwa mtu yeyote kujialika katika nchi nyingine kiholela.

Bunge hilo la Afrika lina jukumu la kutoa ushauri kwa Umoja wa Afrika.