1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Jaji aamuru jina la Trump kubaki kwenye karatasi za kura.

19 Januari 2024

Jaji wa mahakama moja mjini Washington ameamuru jina la rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, liendelee kubakia kwenye karatasi za kura ya uteuzi wa mgombea urais kwa chama cha Republican.

https://p.dw.com/p/4bRZi
Marekani | Mgombea wa uchaguzi kupitia Republican akiwa Iowa | Donald Trump
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ambaye anagombea tena nafasi hiyo kupitia chama ca Republican akiwa kwenye moja ya dhifa za chama huko Des Moines, Iowa, Januari 15, 2024Picha: Andrew Harnik/AP/picture alliance

Katika hukumu hiyo iliyosomwa jana, Jaji Mary Sue Wilson wa Kaunti ya Thurston, alisema msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Washington alitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, pale alipoyakubali majina yote ya wagombea yaliyowasilishwa na vyama vya Republican na Democrat.

Kama ilivyokuwa kwenye majimbo mengine, wapigakura walioweka zuio lao Washington wanadai kuwa Trump hafai kuwania urais kutokana na matendo yake kwenye tukio la tarehe 6 Januari 2021, ambapo hotuba yake kali iliwachochea wafuasi wake kulivamia jengo la bunge kwa lengo la kupinduwa matokeo ya uchaguzi wa 2020.

Mabadiliko ya 14 ya katiba ya Marekani yanapiga marufuku mtu aliyehusika na uasi kushikilia ofisi ya umma. Tayari Trump amezuiwa kwenye majimbo ya Maine na Colorado kuwania urais.