1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Niger

Wanajeshi wa mwisho wa Marekani waondoka Niger

Sylvia Mwehozi
6 Agosti 2024

Jeshi la Marekani limetangaza kukamilisha zoezi la kuwaondoa wanajeshi wake katika kambi ya mwisho nchini Niger, ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja baada ya viongozi wa mapinduzi kutaka wanajeshi wa Washington kuondoka.

https://p.dw.com/p/4j8xt
Wanajeshi wa Marekani wakitoa mafunzo kwa wanajeshi wa Niger
Wanajeshi wa Marekani wakitoa mafunzo kwa wanajeshi wa NigerPicha: Alex Fox Echols Iii/Planetpix/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Jeshi la Marekani limetangaza kukamilisha zoezi la kuwaondoa wanajeshi wake katika kambi ya mwisho nchini Niger, ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja baada ya viongozi wa mapinduzi katika nchi hiyo kutaka wanajeshi wa Washington kuondoka.

Wanajeshi wapatao 800 waliondoka katika kambi ya mjini Niamey mapema mwezi Julai, huku wengine karibu 200 wakisalia katika kambi kubwa ya Agadez kaskazini mwa Niger.

Taarifa iliyotolewa na wizara ya ulinzi ya Marekani imesema zoezi la kuviondosha vikosi vyake na mali katika kambi ya anga ya 201 huko Agadez limekamilika.Marekani yaanza kuondoa wanajeshi wake nchini Niger

Tangu mapinduzi ya mwaka 2023, utawala wa kijeshi wa Niger umeimarisha ushirikiano na majirani zake Mali na Burkina Faso ambazo pia zimeshuhudia mapinduzi na kuwafukuza wanajeshi wa Marekani na Ufaransa. Mataifa hayo matatu yanayoongozwa na jeshi yameunda shirikisho la nchi za Sahel.

Niger Niamey 2024
Maafisa wa kijeshi wa Marekani na Niger Machi 2024Picha: ISSIFOU DJIBO/EPA

Bado kumesalia wanajeshi wachache wa Kimarekani huko Niger ambao kwa kiasi kikubwa wanashughulika na majukumu ya kiutawala yanayohusiana na kuondoka kwao, kulingana na msemaji wa Pentagon Sabrina Singh. Maafisa hao wanafanya kazi katika ubalozi wa Marekani.

Niger imekuwa ikichukuliwa kama mojawapo ya nchi za mwisho katika kanda hiyo ambayo mataifa ya magharibi yamekuwa yakitumai kushirikiana nayo kupambana na uasi wa wapiganaji wenye itikadi kali.Mataifa matano ya kanda ya Sahel yatekeleza luteka ya kijeshi magharibi mwa Niger kuyakabili makundi ya kigaidi

Marekani na Ufaransa zilikuwa na maafisa zaidi ya 2500 wa kijeshi katika ukanda huo hadi kufikia sasa.

Kwa kushirikiana na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya ziliwekeza mamia ya mamilioni ya dola katika usaidizi wa kijeshi na mafunzo. Mnamo mwezi Aprili, wakufunzi wa kijeshi wa Urusiwaliwasili huko Niger ili kuimarisha mfumo wa anga wa nchi hiyo.