1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Mali latwaa udhibiti wa ngome muhimu ya waasi,Kidal

15 Novemba 2023

Waasi Wakituareg wameukimbia mji wa Kidal baada ya kukubali kushindwa na jeshi katika mapambano makali

https://p.dw.com/p/4YpIl
Assimi Goita akishiriki gwaride la kijeshi siku ya maadhimisho ya Uhuru Septemba 22.2022 mjini Bamako
Kiongozi wa utawala wa kijeshi wa Mali Luteni Kanali Assimi Goita katikatiPicha: AP Photo/picture alliance

Jeshi nchini Mali limetoa mwito wa utulivu baada ya kuukomboa mji wa  Kidal ulioko kaskazini mwa nchi na iliyokuwa ngome muhimu ya waasi wa kabila la Tuareg. Jeshi limesema limeshachukuwa hatua za kuhakikisha usalama wa wakaazi wa mji huo, na kuwataka waliheshimu jeshi.

Kidal mji wa kimkakati

Mji wa Kidal ni mji muhimu wa kimkakati kwa jeshi la Mali katika upande wa Kaskazini mwa nchi hiyo na kwa miaka umekuwa ukidhibitiwa na kundi la waasi wa Kituareg wanaopigania kuwa na utawala wao na kujitenga na Mali, suala ambalo limekuwa likizusha mvutano mkubwa. Jeshi kuudhibiti mji wa Kidal kwa hivyo ni ishara kubwa ya mafanikio kwa viongozi wa utawala wa kijeshi mjini Bamako walioingia madarakani mwaka 2020.

Mwanajeshi wa Mali akiwa kazini
Mwanajeshi wa Mali akiwa na bunduki aina ya AK-47 akiwa doria kati ya mji wa Gao na Kidal,mwezi JulaiPicha: KENZO TRIBOUILLARD/AFP/Getty Images

Na hilo limeonekana jana mara baada ya kiongozi wa utawala huo wa kijeshi, Kanali Assimi Goita kuthibitisha juu ya kukombolewa mji huo, inaelezwa mamia ya watu walimiminika katika uwanja wa Uhuru mjini Bamako wakishangilia,huku wakipeperusha bendera za nchi yao na kulimwagia sifa jeshi la taifa.Mmoja ya walioandamana amesema hivi

"Huu nisingeuita ushindi, Ushindi siku zote ulikuweko upande wetu,japo waliotutangulia walikuwa ni wasaliti,Sikuwahi hata mara moja kulitilia shaka jeshi letu. Nilijuwa tu kwamba hiki kitatokea siku moja na siku hiyo ni Novemba 14 mwaka 2023.Ni siku itakayoingia kwenye vitabu vya historia ya Mali''

Jeshi la Mali lilitwaa udhibiti wa mji wa Kidal jana Jumanne baada ya kutokea mapigano makali yaliyosababisha mamia ya wakaazi wa Kidal kukimbia kabla hata jeshi halijaingia kwenye mji huo.

Mapambano ya kuwania Kidal

Kikosi kikubwa cha wanajeshi kilichokuwa kimekita kambi tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba katika kijiji cha Anefis, umbali wa kilomita 110 kutoka Kusini mwa Kidal, walianza kuusogelea mji huo tangu mwishoni mwa juma.Soma pia: Mali: Mzozo wa Tuareg wazuka tena

Kikosi hicho kikisaidiwa na ndege za kivita kilikabiliwa na mashambulizi makali kutoka upande wa waasi na kiongozi wa jeshi hilo la Mali waasi wengi waliuwawa kwenye operesheni hiyo. Muungano wa kimkakati wa waasi CSP unaojumuisha zaidi makundi ya wapiganaji wakituareg limekiri kushindwa na kusema limeondoka Kidal kwa kile ilichokiita ni kwa sababu za kimkakati. Kundi hilo limesema kwamba bado mapambano yake yanaendelea.

Waasi wa Kituareg wanapigania kujitenga kwa  eneo la Kaskazini mwa Mali
Kundi la waasi wa Mali la harakati za ukombozi wa AZAWAD CMA likipiga doria mjini Kidal Agosti mwaka 2022Picha: SOULEYMANE AG ANARA/AFP/Getty Images

Jeshi la Mali na serikali mjini Bamako kwa miaka wameshindwa kufanikiwa kuutwaa mji wa Kidal, ukiwa mikononi mwa makundi ya Kituareg lakini utawala wa kijeshi ulionesha kwa muda mrefu juhudi zake za kutaka kuukomboa mji huo. 

Baada ya mafanikio ya kuutwaa mji huo, jeshi limesisitiza kwamba mapambano hayajamalizika likikumbusha kwamba mapambano yao yanajumuisha hatua ya kukomboa na kurudisha uthabiti wa eneo zima hilo la Kaskazini. Wakati jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa MINUSMA lilipoondoka kwenye kambi zao mjini Kidal Oktoba 31 waasi Wakituareg mara moja walizidhibiti kambi hizo.

Soma pia: UN yaondoka Mali kwa wasiwasi huku ghasia zikiongezekaTangu mwezi Julai ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa umeshaondowa wanajeshi na wafanyakazi wake kiasi 6000 baada ya utawala mjini Bamako kuutaka ujumbe huo uondoke nchini Mali. Na tarehe ya mwisho ya kuondoka iliyotangazwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ni Desemba 31.

Ujumbe wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa,Mali
Ujumbe wa MINUSMAPicha: Nicolas Remene/Le Pictorium/MAXPPP/dpa/picture alliance

Waasi wa Kituareg hawataki MINUSMA wakabidhi kambi zao kwa jeshi la Mali wakisema hatua hiyo inakwenda kinyume na makubaliano yaliyofikiwa huko nyuma pamoja na serikali ya kuweka amani.

Ikumbukwe kwamba Jeshi la Mali liliwahi kupata pigo kubwa sana kwa kushindwa mara mbili katika vita ya kuutetea mji huo mwaka 2012 na 2014 na matukio hayo yakawa ndo chanzo cha kuandamwa na matatizo kwa serikali mjini Bamako. Na viongozi wa sasa walioko madarakani katika utawala wa kijeshi waliapa kuukomboa mji huo.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW