1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Israel lasema laendesha shughuli zake Gaza

Josephat Charo
8 Novemba 2023

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Gaza na wanaongeza shinikizo dhidi ya kundi la Hamas lililotambuliwa kuwa la kigaidi nchini Ujerumani, Marekani na Umoja wa Ulaya, kila saa na kila siku.

https://p.dw.com/p/4YXOQ
Gazastreifen | Israelische Armee
Wanajeshi wa Israel waendelea kulishinikiza kundi la Hamas kila baada ya saa na siku.Picha: Israeli Defense Forces/Handout via REUTERS

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema mji huo umezingirwa. Akizungumza katika taarifa iliyoonyeshwa kwenye televisheni Netanyahu amesema wanaongeza shinikizo dhidi ya kundi la Hamas lililotambuliwa kuwa la kigaidi nchini Ujerumani, Marekani na Umoja wa Ulaya, kila saa na kila siku. Netanyahu pia amesema kufikia sasa wamewaua maalfu ya magaidi ardhini na chini ya ardhi.

Kwa mara nyingine Netanyahu amesema usitishwaji mapigano au kuanza tena upelekaji mafuta ni masuala ambayo hayazingatiwi kwa sasa mpaka Hamas watakapowaachia huru mateka waliosalia. Amerudia wito wake kwa raia wahamie kusini mwa Ukanda wa Gaza kuepusha mapigano.

Wakati huo huo, waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant amesema wanajeshi wa Israel wanaendesha harakati eneo la katikati ya mji wa Gaza lenye idadi kubwa ya watu. Amesema kiongozi wa cheo cha juu wa Hamas, Yahya Sinwar, ametengwa kwenye handaki lake huku wanajeshi wa Israel wakiendelea kukaza kamba kuuzunguka mji wa Gaza.

Maafisa wa serikali ya Israel walikuwa wakizungumza mwezi mmoja tangu shambulizi la kigaidi la Hamas la Oktoba 7 nchini Israel lililowaua watu takriban 1,400 na kusababisha mgogoro wa mpakani.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia utoaji wa misaada ya kibinadamu katika ardhi ya Wapalestina, UNRWA limesema mfanyakazi wake mwingine mmoja ameuliwa na mwingine kujeruhiwa vibaya katika kipindi cha saa 24 zilizopita. Shirika hilo limesema jumla ya maafisa wake 89 wameuwawa na wengine wapatao 26 kujeruhiwa tangu vita kati ya Israel na Hamas vilipozuka. UNRWA imesema hii ndio idadi kubwa ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kuuliwa katika historia ya umoja huo.

Israel Gaza Israelisch-palästinensischer Konflikt – Khan Yunis
Muokoaji wa Kipalestina akimsafirisha muhanga aliyepatikana chini ya vifusi vya jengo lililoharibiwa kufuatia shambulizi la kutokea angani la Israel, kusini mwa GazaPicha: Mohammed Talatene/dpa/picture alliance

Wiki hii shirika hilo lilisema takriban watu milioni 1.5 wamelazimika kuyahama makazi yao huko Gaza kutokana na vita hivyo, ikiwa ni sawa na takriban asilimia 70 ya idadi jumla ya wakazi. Karibu nusu yao walikuwa wamepewa hifadhi na wanaishi katika maeneo ya shirika la UNRWA, sana sana katika shule. Taarifa ya shirika hilo imesema kiasi vituo 50 vimeathiriwa tangu mzozo ulipozuka na mtu mmoja aliyekuwa ameyahama makazi yake aliuliwa na wengine tisa kujeruhiwa katika kituo kimoja kaskazini mwa Ukanda wa Gaza siku ya Jumatatu baada ya kulengwa moja moja katika mashambulizi.

Waandishi wa habari 41 wameuliwa tangu mzozo wa Gaza kuanza

Shirika la waandishi habari wasio na mipaka, Reporters Without Borders, RSF, limesema limerekodi vifo 41 vya waandishi habari tangu mashambulizi ya kigaidi ya kundi la Hamas Oktoba 7 nchni Israel na hatua za kulipiza kisasi za Israel katika Ukanda wa Gaza. Shirika hilo limetoa wito waandishi wote huko Gaza walindwe na waandishi wa kigeni waruhusiwe kuingia na kufanya kazi kwa uhuru.

Kwa mujibu wa shirika la waandishi habari wasio na mipaka jumla ya waandishi 36 wameuliwa Gaza na linaweza kuthibitisha kwamba angalu 10 kati yao walikuwa wanafanya kazi ya kuripoti habari wakati walipokufa. Ripota mmoja aliuliwa nchini Lebanon siku za mwanzo za vita vya Gaza na waandishi wanne wa Israel waliuliwa katika shambulizi la Hamas Oktoba 7.

Wakati haya yakiarifiwa mshauri wa cheo cha juu wa rais wa Marekani Joe Biden, Amos Hochstein, amefanya ziara ambayo haikutangazwa mjini Beirut kwa ajili ya mazungumzo na spika wa bunge la Lebanon na waziri mkuu wa mpito. Hochstein amewaambia waandishi wa habari baada ya kukutana na spika Nabih Berri kwamba kurejesha utulivu katika mpaka wa kusini wa Lebanon ni suala la umuhimu mkubwa.

Katika taarifa fupi Hochstein amesema Marekani haitaki kuona mzozo wa Gaza unaendelea na kutanuka hadi Lebanon. Hakuruhusu maswali kutoka kwa waandishi habari. Matamshi yake yanakuja wakati jeshi la Israel na wanamgambo wa kundi la Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran wakipambana katika ufyetulianaji wa risasi mpakani.

(dpae,ape)