1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Kiongozi wa jeshi la Sudan akataa upatanisho na RSF

6 Januari 2024

Jenerali wa vikosi vya Sudan Abdel Fattah al-Burhan ameapa kuendeleza vita vilivyodumu kwa miezi tisa kati ya jeshi la wanamgambo wa RSF, huku akizikataa juhudi za hivi karibuni za suluhu.

https://p.dw.com/p/4av2u
Sudan | Jeneral Abdel Fattah Al-Burhan
Picha ya video iliyotolewa katika ukurasa wa Facebook wa jeshi la Sudan mnamo Agosti 14, 2023 ikimuonyesha mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan akitoa hotuba. Kiongozi huyo anasema hatakubali kusuluhishwa na RSF Picha: Sudanese Army/AFP

Burhan amesema ulimwengu mzima umeshuhudia namna waasi hao walivyofanya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu huko Darfur Mashariki na kwingineko nchini Sudan.

Amewaambia wanajeshi waliokuwa wamekusanyika huko Port Sudan kwamba ni kwa sababu hiyo, hawatakubali kupatanishwa na wala hakutakuwa na makubaliano.

Kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo amapema wiki hii alikubali kusitisha mapigano, kufuatia pendekezo la makundi ya kiraia, ingawa waangalizi walilionyesha wasiwasi kwa kuzingatia historia ya RSF ya kutotekeleza ahadi zake.

Hata kwenye mazungumzo yake na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, mjini Pretoria Daglo alisema yuko tayari kusitisha mapigano na kuvimaliza vita ambavyo vimeiharibu nchi yake. 

Kulingana na Umoja wa Mataifa, mapigano ya Sudan yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 12,000 huku wengine zaidi ya milioni 7 wamelazimika kuyakimbia makaazi yao.