1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jean-Marie Guehenno wa Umoja wa Mataifa amaliza muhula wake

Kalyango Siraj30 Julai 2008

Ameongoza idara ya kikosi cha kulinda amani kwa miaka minane

https://p.dw.com/p/Emzh
Askari wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa wakiwa katika kazi ya ulinzi barani AfrikaPicha: AP

Mkuu wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani-Jean-Marie Guehenno anamaliza muhula wake mwezi huu,wakati akiwa na wasiwasi wa askari wa Umoja wa Mataifa kutumwa nchini Somalia.

Wasiwasi wake unatokana na kutojua nani anaedhibiti wapiganaji wa chini kwa chini nchini humo.

Bwana Jean-Marie Guehenno, mwanadiplomasia wa Ufaransa amekuwa akiingoza idara ya kikosi cha kulinda amani ya Umoja Mataifa kwa kipindi cha miaka minane.Na wakati wake wa kustaafu ndio umefika.

Lakini anaondoka wakati idara hiyo ikitaka kutuma vikosi vyake nchini Somalia ambayo imekuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mda mrefu.

Jean-Marie Gueheno alisema jana kuwa ana wasiwasi na kutumwa kikosi nchini somalia wakati haujulikani nani anadhibiti makundi kadhaa ya wapiganaji huko.

Mapigano kati ya vikosi vya serikali ya mpito dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu yamesababisha vifo vya watu kawaida zaidi ya 8,000 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, huku wengine millioni moja kuachwa bila ya makazi.

Pande mbili muhimu katika mgogoro wa Somalia yaani serikali ya mpito na wapinzani walioko uhamishoni, ziliafikiana nchini Djibout mwezi jana miongoni mwa mengine kutaka kutumwa vikosi vya Umoja wa Mataifa na pia kuahidi kusitisha hujuma dhidi ya upande mwingine baada ya mwezi mmoja.

hata hivyo makubaliano yalipingwa na kiongozi mmoja wa kisomali mwenye msimamo mkali Sheikh Hassan Dahir Aweys.

Sheikh Aweys hivi juzi alidaiwa kuchukua uongozi wa chama cha upinzani cha ushirika wa kuikomboa tena Somalia ARS.

Jean-Marie Guehenno,amesema kuwa mwelekeo wa siasa nchini Somalia haueleweki. Aliongeza kwa kujuliza wale wanaotia saini mikataba huko wanaushawishi upi na wanadhibiti silaha kiasi gani?

Bila kupewa jibu aliendelea kuwa ikiwa udhibiti wa silaha wa kundi moja ni mdogo sana ,hii ina maana mikataba inayatiwa saini haiwezi kuwa imara na msingi tosha kwa kuwezesha kutuma kikosi cha kulinda amani huko.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa linasitasita kutuma vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa mataifa nchini Somalia ,mababe wa kivita, wapiganaji wa kiislamu wamekuwa wakipigana dhidi ya serikali ya Somalia inayosaidiwa na Ethiopia.

Nao Umoja wa Afrika unasema kuwa vikosi vyake vya kulinda amani huko hawiwezi peke yake kutuliza hali ya mambo na hivyo kuomba msaada wa vikosi vya Umoja wa Mataifa.

Licha ya shaka zake kuhusu Somalia hata hivyo Jean-Marie Guehenno amesema kuwa ni vigumu kukataa kutuma vikosi vya kulinda mani huko kwani haiwezekani kusema hapana ikiwa wewe tu ndie silaha ya mwisho.