1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je uvamizi wa Marekani Afghanistan uliibadilisha taifa hilo?

7 Oktoba 2021

Miaka 20 iliyopita, Marekani iliivamia kijeshi Afghanistan na kuuangusha utawala ya itikadi kali wa kundi la Taliban. Miaka 20 baadae kundi hilo limerejea madarakani, lakini je Afghanistan ni sawa na ilivyokuwa zamani?

https://p.dw.com/p/41PTZ
US-Soldaten in Kuwait
Picha: picture-alliance/L. Rauch

Tarehe kama ya leo Oktoba 7 mwaka 2001, Marekani iliivamia Afghanistan ili kulipiza kisasi mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11 yaliopangwa na kundi la Al Qaida ndani ya taifa lake.

Lengo hasa la uvamizi wa Marekani ni kumsaka kiongozi wa kundi hilo Osama Bin Laden na kuliadhibu kundi la Taliban kwa kutoa mahala salama kwa viongozi wa al Qaida.

Haikuwa kazi kubwa kwa Marekani kuusambaratisha utawala wa Taliban. Hata hivyo Osama Bin Laden alifanikiwa kutoroka, lakini baadaye alisakwa na kuuwawa na vikosi vya Marekani nchini Pakistan mwaka 2011.

soma zaidi: Borrell: Sera za Taliban zinakwamisha msaada kwa Afghanistan

Uvamizi huo ulifanikiwa kwa kiasi kikubwa, japokuwa wapiganaji wa Taliban na Alqaida walifanikiwa pia kujikusanya upya baada ya miaka kadhaa kutokana na mataifa ya Magharibi, kuiunga mkono serikali ya Hamid Karzai iliyoingia madarakani. Mwaka 2005, Taliban ilijiimarisha tena na kuanzisha vuguvugu lililopambana na vikosi vya Jumuiya ya kujihami NATO.

Kwa waafghani walio wengi, uvamizi wa Marekani na kuanguka kwa utawala wa Taliban kulileta mabadiliko chanya. Kulielezea enzi mpya huku wengi wakiwa na matumaini ya taifa lao kuimarika siku za usoni.

Nini kilichoharibika?

Afghanistan Taliban Kämpfer im Vergnügungspark in Qarghah, nah Kabul
Baadhi ya wanachama wa kundi la TalibanPicha: Wakil Kohsar/AFP

Lakini hali haikuwa ya utulivu kwa muda mrefu nchini Afghanistan. Mwaka 2003, Marekani ilijihusisha na vita vya Iraq, ikitumai serikali ya Karzai kwa usaidizi wa vikosi vya kigeni itapambana na uasi na kuiweka Afghanistan katika njia ya kujiimarisha zaidi.

Kwa mujibu wa gazeti la The Times, wakosoaji wa Serikali ya Marekani wakati huo ikiongozwa na rais George Bush, waliamini kuwa vita ya Iraq vilipunguza juhudi za Marekani katika kuiimarisha Afghanistan madai yaliyopingwa na utawala huo.

Kuanzia mwaka 2005, serikali ya Marekani ikaanza kuishutumu Pakistan kutoa mahala salama kwa kundi la Taliban. Kuimarika tena kwa kundi hilo kukaanza kusababisha ghasia za hapa na pale nchini Afghanistan na hali ikaanza kuwa mbaya. 

Akram Arife, mhadhiri katika chuo kikuu cha Kabul ameiambia DW kwamba Marekani tayari ilikuwa imeshaanza kushindwa. Amesema Marekani ilipaswa kujua hakuna suluhu ya kijeshi katika mgogoro wa Afghanistan huku akisisitiza kuwa Marekani ingetafuta mawazo mengine baada ya uvamizi.

Wataalamu wanasema Marekani iliweka nguvu zake zote mjini Kabul na kusahau maeneo mengine ya nchi. Hatimaye Kundi la Taliban likachukua tena madaraka agosti 15 mwaka 2021 bila ya ushindani wowote kutoka kwa vikosi vya serikali ya Ashraf Ghani. Juhudi zote za Marekani baada ya kukaa nchini humo kwa miaka ishirini zikasambaratika.

Wataalamu wanasema nguvu za marekani nchini humo hazikupotea, jamii ya waafghanistan imebadilika tangu uvamizi ulipofanyika, hadi Taliban inalazimika kubadili muonekano wake kwa jamii ya Kimataifa.

Baada ya kuudhibiti mji wa Kabul, Taliban imesema inataka kuunda serikali itakayowashirikisha wote na kwamba utawala mpya utakuwa tofauti kuliko ule uliokuwepo kabla ya uvamizi wa Marekani.

Mwandishi: Amina Abubakar