1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Wamarekani wenye asili ya kiarabu wana matumaini na Trump?

Bakari Ubena Janelle Dumalaon
2 Januari 2025

Wakati Donald Trump akijiandaa Januari 20 kuingia katika ikulu ya White House, Wamarekani wenye asili ya kiarabu wanafuatilia kwa makini uteuzi wa serikali yake huku kukiwa na mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/4olSu
Rais mteule wa Marekani Donald Trump
Rais mteule wa Marekani Donald TrumpPicha: Cheney Orr/REUTERS

Wamarekani wwnye asili ya kiarabu wanazingatia urithi wa sera za zamani za Trump na uungaji wake mkono usiyosumba kwa Israeli na jinsi yote hayo yanaweza kuathiri sera ya Marekani.

Wakati wa kampeni zake, Rais mteule wa Marekani Donald Trump aliungwa mkono na Wamarekani wenye asili ya Uarabu katika baadhi ya majimbo. Kwa mfano Wasel Yousaf ambaye alifanikiwa kupiga picha na Trump aliyezunguukwa na wafuasi wenye asili ya Kiarabu huko Dearborn, Michigan.

Hata hivyo, itakumbukwa kuwa kuna wakati Trump hakuashiria matumaini kwa Wamarekani Waarabu au Wamarekani Waislamu. Muda mfupi baada ya kuingia madarakani mwaka 2017, kiongozi huyo alitia saini sheria iliyopiga marufuku raia wa kigeni kutoka nchi saba zenye Waislamu wengi kuingia Marekani, hatua ambayo wakosoaji wake waliiita kuwa ya "kupiga marufuku Waislamu."

Mtu akionyesha pasi yake ya kusafiria ambayo visa yake ya Marekani ikiwa imefutwa
Mohammed Al Zabidi akionyesha pasi yake ya kusafiria ambayo visa yake ya kuishi Marekani ikiwa imefutwaPicha: Hani Mohammed/AP Photo/picture alliance

Wakati wa kampeni za urais za mwaka 2024, Trump alisema atairejesha marufuku hiyo ya kusafiri na kuitanua zaidi ili kuwazuia wakimbizi kutoka maeneo yaliyokumbwa na ugaidi kama vile Ukanda wa Gaza.

Soma pia: Hotuba ya rais Donald Trump juu ya Uislamu

Mzozo wa Mashariki ya Kati na kukatishwa tamaa na utawala wa Rais Joe Biden ulipelekea Wamarekani wengi wenye asili ya Kiarabu kupiga kura kwenye uchaguzi huko Dearborn, jiji lenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu nchini Marekani. Wengi walisema walisikitishwa na kushindwa kwa Biden kudhibiti mashambulizi ya Israel huko Gaza.

"Amani kwa kutumia nguvu"

Yousaf amesema jamii nyingi za Waarabu nchini Marekani zinazingatia mila na desturi za nchi zao na ndio maana wanatafuta amani. Ameongeza kuwa kampeni za Trump ziliashiria amani kupitia nguvu na matumaini ya kuona vita kote ulimwenguni ikiwa ni pamoja na Ukraine, Gaza, Yemen na Syria vinamalizika.

Soma pia: “Sisi pia ni Wamarekani“: Maisha na taswira ya Muislamu nchini Marekani baada Septemba 11

Katika mahojiano yake ya kwanza tangu kuchaguliwa tena, yaliyopeperushwa Disemba 8 mwaka jana katika kipindi cha "Meet the Press" cha shirika la habari la NBC, Trump alipohojiwa iwapo atamshinikiza Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kumaliza vita huko Gaza, alisema anataka vita hivyo visitishwe lakini lazima kuwe na ushindi wa Israel. Wakati wa kampeni, Trump aliahidi amani Mashariki ya Kati lakini hakueleza mpango ulio wazi wa jinsi ya kulifanikisha hilo.

"Vita haviwezi kuendelea milele"

Wanawake wakipinga sheria ya Trump ya kuwazuia watu kutoka mataifa yenye waislamu wengi kuingia Marekani
Wanawake wakipinga sheria ya Trump ya kuwazuia watu kutoka mataifa yenye waislamu wengi kuingia MarekaniPicha: Ronen Tivony/ZUMA Press/IMAGO

Bilal Irfan, mwanafunzi anayesomea udaktari ambaye alitumia muda wake wa mapumziko ya kiangazi kwa shughuli za kujitolea katika shule za Ukingo wa Magharibi, amesema pia kuwa na matumaini kwamba vita vitakwisha hivi karibuni, lakini akasisitiza kuwa si serikali ya Marekani  iwe inayoondoka au inayokuja itakayoweza kufanikisha hilo. Irfan ameendelea kuwa ikiwa serikali ya Marekani haitokuwa na mabadiliko makubwa kwenye sera yake kuihusu Israel, basi nchi hiyo itaendelea na mauaji yake Gaza kwa namna na muda itakayo licha ya kuwa ana imani kuwa vita haviwezi kuendelea milele.

Hivi karibuni, shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International lilisema kuwa Israel inaendesha "mauaji ya halaiki" huko Gaza. Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ  ilishaeleza kuhusu uwezekano kwamba Israel ilikiuka masharti ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari, matamshi ambayo yalikanushwa vikali na Israel na washirika wake ikiwa ni pamoja na Ujerumani na Marekani.

(DW)