1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je kikosi cha Umoja wa Ulaya kitafaulu kuwalinda wakimbizi nchini Chad

Josephat Charo7 Novemba 2007

Umoja wa Ulaya unataka kutuma kikosi chake mashariki mwa Chad katika mpaka na Sudan ili kuhakikisha usalama wa wakimbizi wengi walio katika eneo hilo, hususan kutoka Darfur nchini Sudan. Kikosi hicho kinachoitwa, EUFOR, kitaongozwa na Ufaransa. Ujerumani lakini ina wasiwasi juu ya kupelekwa kwa kikosi hicho nchini Chad.

https://p.dw.com/p/C7f0
Wakimbizi wa Darfur
Wakimbizi wa DarfurPicha: AP

Rais wa Chad, Iddris Debby, alikubali shingo upande kupelekwa kwa kikosi cha Umoja wa Ulaya mashariki mwa Chad. Kashfa ya shirika la misaada la kifaransa, Arche de Zoe, kuwateka nyara watoto wa Chad imezusha wasiwasi huku ikitishia kuuelekeza pabaya mpango wa Umoja wa Ulaya kupeleka jeshi lake nchini humo.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufaransa alikieleza kitendo cha shirika la Arche de Zoe kuwa cha kuhuzunisha na ambacho huenda kisababishe athari za muda mrefu. Ufaransa ina idadi kubwa ya wanajeshi katika kikosi cha wanajeshi 2,500 kitakachopelekwa Chad mwezi ujao. Ireland na Poland zitapeleka wanajeshi 700 zaidi, Sweden, Ubelgiji, Austria na Uhispania zimeahidi kupeleka idadi ndogo ya wanajeshi.

Mbunge wa chama cha FDP hapa Ujerumani, Karl Addicks, ni msemaji wa ushirikiano wa kiuchumi. Aliunga mkono kupelekwa kwa kikosi cha Umoja wa Ulaya kusaidia kulinda amani wakati wa uchaguzi nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo mwaka jana. Lakini ana wasiwasi kuhusu kupelekwa kikosi cha umoja huo nchini Chad.

´Ninalitazama eneo kutakakopelekwa wanajeshi, yaani kaskazini mwa Chad, eneo la Darfur magharibi mwa Sudan, na kwa muda mfupi pengine eneo la kaskazini mwa Niger, kuwa eneo hatari sana la mgogoro. Nio vigumu kufahamau mtu alipo. Baadhi ya makundi ya waasi hayako tayari kujitambulisha mara moja. Ndiyo sababu kwa nini nashauri majeshi yapelekwe.´

Hali ya kibinadamu ni mbaya mno katika mpaka wa Chad na Sudan na matatizo hayana mpaka. Takriban wakimbizi kati ya milioni mbili na milioni tatu wanakabiliwa na hali ngumu katika jimbo la Darfur na idai kubwa kati yao wamekimbilia nchini Chad kutafuta usalama. Lakini hata huko wanahofia kushambuliwa na makundi ya waasi na tayari maelfu ya wakimbizi wameuwawa.

Jambo la kushangaza ni kwamba serikali ya Sudan na Chad hazina nia ya kutafuta amani. Ndio maana mjumbe wa muungano wa CDU-CSU anayehusika na maswala ya Afrika, Hartwig Fischer, anapinga wanajeshi wa Ujerumani kutumwa kushiriki katika harakati za kijeshi.

´Hali ni ngumu katika eneo hilo kwa kuwa mtu anaweza kujikuta katikati mwa makundi yanayopigana. Hali ni tete huku waasi wakiwa wanapigana wenyewe kwa wenyewe, waasi wanapigana na majeshi ya serikali na serikali inapigana dhidi ya waasi. Kwa hiyo hali ni mbaya mno.´

Nchini Chad, kama koloni za zamani za Ufaransa barani Afrika, kuna upinzani mkali dhidi ya Ufaransa. Nchini Ivory Coast, Togo na sasa Chad, maandamano ya kuipinga Ufaransa yamekuwa yakifanywa mara kwa mara. Kwa kuzingatia hali hii, huenda uongozi wa Ufaransa wa kikosi cha Umoja wa Ulaya nchini Chad ukaleta matatizo.

´Naamini hatujafaidika kwamba jukumu limo mikononi mwa Ufaransa kwa sababu kuna upinzani mwingi dhidi ya Ufaransa katika eneo hilo. Kwa upande mwingine rais wa Sudan Omar al Bashir hana haja na kuumaliza mgogoro huo, na nchini Chad hali imekuwa mbaya. Chad pia haiungi mkono kupelekwa tume ya Umoja wa Mataifa kulinda amani Darfur.´

Ikizingatiwa hali ilivyo, kikosi cha Umoja wa Ulaya huenda kikafaulu kutimiza machache kati ya malengo yake. Ujerumani haitalenga kuwapeleka wanajeshi wake Chad lakini itatoa msaada wa uratibu. Ni ukweli ulio uchungu kwamba Chad na Sudan hazina haja ya kutafuta suluhisho la mzozo na makundi yanayopigana bado hayajachoka. Kuna wasiwasi ikiwa kikosi cha Umoja wa Ulaya nchini Chad kitafaulu.