1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Italia yaomba UN ichunguze mauaji ya balozi wake DRC

Angela Mdungu
24 Februari 2021

Italia imeuomba Umoja wa mataifa uazishe uchunguzi kuhusu mauaji ya balozi wake katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Luca Attanasio

https://p.dw.com/p/3poBP
Italien Regierungsbildung | Luigi Di Maio
Picha: picture-alliance/AP/A. Carconi

Mwakilishi huyo wa Italia, aliuwawa Jumatatu baada ya msafara wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP kushambuliwa ghafla katika eneo hatari linalopakana na Rwanda mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasi ya Congo.

Katika shambulio hilo, dereva wa mwakilishi huyo ambaye pia ni raia wa wa Italia aliuawa.  Waziri wa mambo ya kigeni wa Italia, Luigi Di Maio, aliliambia bunge la nchi yake kuwa wamewasilisha rasmi ombi kwa shirika la mpango wa chakula duniani pamoja na umoja wa mataifa  kuanzisha upelelezi utakaobainisha klichotokea, hatua za kiusalama zilizochukuliwa na kubaini ni nani hasa aliyehusika na ukatili huo.

Akielezea kuhuzunishwa kwake na mauaji ya balozi Attanasio, waziri wa mambo za kigeni wa Italia amesema Ujumbe WFP ulialikwa na Umoja wa Mataifa, kwa hivyo ratiba yao iliyoendelea kwa gari ilifanyika ndani ya mpango kazi ulioratibiwa shirika hilo la mpango wa chakula duniani.

Kwa sababu hiyo ameliomba shirika la WFP mjini Roma na Umoja wa Mataifa, kwa kumhusisha moja kwa moja katibu mkuu wa umoja wa mataifa Antonio Giterres, watoe ripoti ya kina juu ya shambulizi dhidi ya msafara huo.

Di Maio  ametoa kauli hiyo baada ya miili ya raia hao wawili wa Italia kurejeshwa nchini humo. Awali, waziri wa mambo ya ndani wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo alilitupia lawama kundi la waasi wa  nchi jirani ya Rwanda la FDLR kwa kuhusika na tukio hilo. Hata hivyo kundi hilo limekanusha kuhusika na mauaji hayo na kuwanyooshea kidole cha lawama wanajeshi wa Rwanda na DRC kuwa ndiyo waliohusika.

Aeleza shambulio lilivyofanywa

Di Maio katika hotuba yake kwa jopo la wabunge, alitoa maelezo ya awali ya namna shambulio hilo lilivyofanywa  akisema washambuliaji sita wanadaiwa kuwa waliyaamuru magari katika msafara huo kusimama kwa kuweka vizuizi barabarani na kisha walifyatua risasi kadhaa hewani.

Italienischen Botschafters im Kongo, Luca Attanasio
Balozi wa Italia aliyeuwawa DRC Luca AttanasioPicha: AFP/Italy's Foreign Ministry

Akinukuu maelezo ya gavana wa Kivu Kaskazini, Di Maio amesema, ingawa milio ya risasi iliwavuta walinzi wa mbuga ya Virunga na wanajeshi, wavamizi hao waliwaamuru watu waliokuwa kwenye msafara huo watoke nje na kuingia vichakani kisha wakamuua dereva wa WFP.

Ameeleza kuwa, walinzi wa mbuga waliokuwa na silaha walipowasili eneo la tukio, wavamizi walianza kurusha risasi na kumlenga balozi aliyejeruhiwa vibaya na kisha kupelekwa hospitalini Goma ambapo ndipo umauti ulipomkuta.

Hivi karibuni ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kideomokrasia ya Congo ilitangaza kuwa  mabalozi wote nchini humo watapaswa kuripoti kwa serikali mienendo yao yote ndani ya nchi hiyo.