1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Italia: Bunge laamua kumwondolea kinga Matteo Salvini

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
12 Februari 2020

Wabunge wa Italia wamepitisha hatua ya kumwondolea kinga kiongozi wa chama cha Lega cha mrengo mkali wa kulia Matteo Salvini.

https://p.dw.com/p/3XgNQ
Italien Padua Matteo Salvini
Picha: Getty Images/AFP/M. Bertorello

Matteo Salvini aliyekuwa zamani waziri wa mambo ya ndani wa Italia anatuhumiwa kwamba aliwazuia kinyume cha sheria wahamiaji waliotaka kuingia nchini Italia bila vibali kwa kupitia njia ya baharini mnamo mwaka jana. Matokeo rasmi ya kura hiyo yanatarajiwa kutangazwa rasmi baadae lakini kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters ni kwamba matokeo ya awali tayari yameonyesha wabunge wengi wameunga mkono hatua hiyo ya kumwondolea kinga waziri huyo wa zamani wa mambo ya ndani wa Italia.

Uamuzi huo sasa unawawezesha waendesha mashtaka mjini Sicily kumfungulia kesi bwana Salvini kutokana na uamuzi wake wa kuwazuia wahamiaji 131 wliokuwa ndani ya meli ya uokozi kwa muda wa siku sita mnamo mwezi Julai mwaka uliopita wakati alipokuwa akisubiria nchi zingine za Jumuiya ya Ulaya zikubaliane juu ya kuwachukua wahamiaji hao.

Matteo Salvini, anaweza kukabiliwa na adhabu ya kifungo cha hadi miaka 15 jela iwapo atapatikana na hatia. Iwapo atahukumiwa hatua hiyo itamzuia kushikilia ofisi yoyote ya kisiasa na hivyo kuvuruga matarajio yake ya kuiongoza serikali ya Italia hapo baadaye.

Kwa mujibu wa katiba ya Italia, bunge linaweza kuzuia kesi zilizopo mahakamani iwapo wabunge watahisi kwamba waziri alikuwa anatimiza majukumu yake kwa kuzingatia maslahi ya kitaifa. Waziri wa mambo ya ndani anaweza kuzuia au kukataza vyombo vya baharini kuingia au kupitia bahari ya Italia kwa kuzingatia misingi ya usalama wa umma, isipokuwa katika matukio yanayohusisha vyombo vya majini vya kijeshi au meli za walinzi wa pwani.

Vyanzo: RTRE/AFP