1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yazidisha mashambulizi baada ya askari wake kuuawa

Sylvia Mwehozi
24 Januari 2024

Israel imeendeleza mashambulizi yake makali katika mji uliozingirwa wa Khan Younis uliopo Ukanda wa Gaza baada ya wanamgambo wa Kipalestina kufanya shambulizi baya zaidi dhidi ya vikosi vya Israel siku ya Jumanne.

https://p.dw.com/p/4bcHq
Askari wa Israel mjini Khan Younis
Askari wa Israel katika operesheni zake Khan YounisPicha: Ohad Zwigenberg/AP/picture alliance

Wanamgambo wa Kipalestina wamefanya shambulizi baya zadi dhidi ya vikosi vya Israel huko Gaza na kuwaua askari 21 wa Israel, tangu uvamizi wa Hamas wa mnamo Oktoba iliyopita ulipochochea vita. Saa chache baadaye jeshi la Israel lilitangaza kwamba vikosi vyake vya ardhini vimeuzingira mji wa kusini wa Khan Younis, ambao ni wa pili kwa ukubwa kwenye Ukanda wa Gaza na moshi mzito mweusi umeshuhudiwa ukifuka wakati maelfu ya Wapalestina wakikimbilia upande wa kusini.

Mashuhuda wamesema kwamba vifaru vya Israel na vikosi vyake vimeingia eneo la karibu la pwani la Muwasi ambalo awali lilikuwa limetangazwa na jeshi kuwa sehemu salama kwa Wapalestina.

Hospitali ya Nasser mjini Khan Younis
Mwanamke akiomboleza huku miili ya Wapalestina waliouawa katika mashambulizi ya Israel ikifikishwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Nasser huko Khan Yunis.Picha: Jehad Alshrafi/Anadolu/picture alliance

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameomboleza vifo vya askari wake ambao wamekufa baada ya wapiganaji wa Hamas kufyetua roketi lililolipua vilipuzi ambavyo wanajeshi wa Israel walikuwa wanaweka kulipua majengo. Netanyahu ameapa kuendeleza mashambulizi hadi pale "ushindi kamili" utakapopatikana, ikiwa ni pamoja na kuliangamiza kundi la Hamas na kuwaokoa mateka zaidi ya 100 ambao bado wanashikiliwa na wanamgambo. 

Soma pia: Jeshi la Israel limeendelea kuushambulia mji wa Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza katika kampeni yake ya kulitokomeza kundi la Hamas

"Tumo katikati mwa vita ambavyo bila ya shaka ni halali, tunapata mafanikio kama vile kuizingira Khan Yunis na pia tumepata hasara kubwa. Tunainamisha vichwa vyetu kuwakumbuka waliokufa, na bado hatuachi kujitahidi kufikia lengo letu la kupata ushindi kamili. Pamoja tutapigana na kwa mapenzi ya Mungu, sote tutashinda", alisema Netanyahu.

Soma ripoti hii: Vita vya Gaza: Je, Wapalestina wataweza kurudi nyumbani?

Hata hivyo Waisraeli wanazidi kuhoji ikiwa nchi hiyo itaweza kufikia malengo hayo ya vita. Wakati mapigano yakizidi kushika kasi, Shirika la misaada ya kiutu la Umoja wa Mataida OCHA, limeripoti kwamba vikosi vya Israel siku ya Jumanne, vilikuwa vimetoa maagizo mapya ya  watu kuhama sehemu ya makaazi ya Khan Yunis, yanayokadriwa kuwa na wakaazi nusu milioni na wengine waliokimbia mapigano. Maagizo hayo yametolewa wakati shirika jingine la Mpango wa Chakula duniani likionya kuwa raia wa Gaza wanakabiliwa "janga kubwa la ukosefu wa usalama wa chakula".

Maandamano ya Israel Tel Aviv
Watu wakiwa wameshikilia mabango yanayoonyesha picha za mateka wakati wa maandamano ya kutaka kuachiliwa kwa mateka waliochukuliwa na wanamgambo wa Hamas.Picha: Leo Correa/AP Photo/picture alliance

Idadi ya waliouawa mzozo wa Gaza: Waliouawa Gaza wapindukia 23,000

Shirika la habari la Palestina Wafa, limeripoti kwamba ofisi ya rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas imeshutumua "masharti hayo hatari" kwa wakaazi kuelekea kusini na kuonya kuwa Israel inakusudia "kuwaondoa Wapalestina kutoka ardhi yao na hivyo kusababisha matokeo yasiyotarajiwa". Vita mjini Gaza vilizuka baada ya shambulizi la kushutukiza lililofanywa na Hamas Oktoba 7 na kuwaua watu zaidi ya 1000 wa Israel, wengi wakiwa ni raia.

Na duru tofauti za vyombo vya habari duniani zinasema kuwa kundi la Hamas limeonyesha nia ya kufanya mazungumzo ya kuwaachia baadhi ya mateka wa Israel. Jarida la Wall Street limeripoti jana likinukuu maafisa wa Misri kuwa Hamas iliwaeleza wapatanishi ya kwamba inaweza kufanya mazungumzo ya kuwaachia mateka wa kike na watoto kwa sharti "muhimu" la kusitisha mapigano.

Hadi sasa Hamas imewaachia mateka 105 wakati wa wiki moja ya usitishaji mapigano mwishoni mwa Novemba mwaka jana ambapo pia wafungwa 240 wa Kipalestina waliachiwa kutoka jela za Israel.

Vyanzo: afp/dpa/ap