1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Watu 13 wauawa Gaza katika mashambulizi ya Israel

18 Julai 2024

Watu 13 wameuawa leo baada ya jeshi la Israel kushambulia kwa mabomu kambi za wakimbizi katikati mwa mji wa Gaza upande wa kaskazini.

https://p.dw.com/p/4iSyU
Ukanda wa Gaza l Mvulana wa Kipalestina akiuza bidhaa mjini Khan Younis
Mvulana wa Kipalestina akiendeleza biashara kwenye vifusi vya majengo yaliyoharibiwa baada ya kushambuliwa na Israeli, wakati mapigano yakiendelea yake na Hamas, huko Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza, Julai 14, 2024.Picha: Mohammed Salem/REUTERS

Katika mashambulio hayo watu sita wameuwawa katika mji wa Zawayda na wengine wamefariki baada ya nyumba moja kushambuliwa katika kambi ya Bureij.

Maafisa wa afya wamesema kwenye mashambulio hayo yaliyolenga kambi za wakimbizi katikati mwa Gaza watu wengine watatu waliokuwa ndani ya gari waliuawa katika mji wa Deir Al-Balah, mji unaowapa hifadhi wakimbizi waliokimbia vita.

Jeshi la Israel limesema katika taarifa kuwa, vikosi vyake vimewaua makamanda wawili waandamizi wa kundi la Islamic Jihad katika mji wa Gaza, akiwemo mmoja aliyeshiriki katika shambulio la Oktoba 7 ndani ya ardhi ya Israel.

Maafisa wa afya na wakaazi wa ukanda huo wameeleza kuwa vifaru vya jeshi la Israel vinaelekea ndani zaidi katika mji wa kusini wa Rafah.