1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yapuuza miito ya kusitisha mashambulizi

20 Mei 2021

Israel imeendelea leo na mfululizo wa mashambulizi ya anga kwenye Ukanda wa Gaza yaliyosababisha kifo cha Mpalestina mmoja na kuwajeruhi wengine kadhaa.

https://p.dw.com/p/3tf4j
Weltspiegel 19.05.2021 | Nahostkonflikt | Gaza Stadt, israelischer Luftangriff
Picha: Mohammed Salem/REUTERS

Hayo yanajiri wakati juhudi za kimataifa zinaongezeka kutuliza makabiliano yanayoendelea.

Mashambulizi hayo mapya yamefanyika baada ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kupuuza shinikizo la Marekani la kutaka kukomesha operesheni ya kijeshi dhidi ya wapiganaji wa kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza ambao wanaendelea kuvurumisha maelfu ya maroketi kuelekea Israel.

Mirupiko mikubwa iliyosababishwa na makombora ya ndege za Israel iliutikisa Ukanda wa Gaza usiku wa kuamkia leo ikililenga eneo la katikati ya mji na mji mwingine wa kusini wa Khan Younis.

Jua lilipochomoza wakaazi wa mji wa Khan Younis walikuwa wakipekua vifusi pamoja na mabaki ya nyumba za familia tano ambazo zimeharibiwa kabisa. Makombora ya ndege za kivita yameupiga pia mtaa wenye shughuli nyingine wa al-Saftawi ambao ni kitovu cha biashara kwenye Ukanda wa Gaza.

Israel imedai kuwa imezishambulia nyumba nne za makamanda wa kundi la Hamas ikilenga kuharibu miundombinu yake ya kijeshi pamoja na hifadhi ya silaha kwenye nyumba moja ya mpiganaji wa Hamas huko Gaza

Netanyahu: Operesheni yetu ya kijeshi inaendelea 

Israel - Palästina-Konflikt
Picha: Jaafar Ashtiyeh/AFP/Getty Images

Netanyahu amekataa katakata wito wa Rais Joe Biden wa kusitisha mapigano ambayo yamesababisha vifo vya mamia ya watu.

Hii ni mara ya kwanza kwa washirika hao wawili kutofautiana hadharani tangu kuanza kwa mapigano wiki iliyopita na hilo linaweza kutatiza juhudi za kimataifa za kutaka kusitishwa kwa mapigano.

Hapo jana Jumatano Netanyahu alisema ingawa anaheshimu "uungaji mkono wa rais wa Marekani" lakini Israel inaendelea na operesheni yake ya kurejesha "utulivu na usalama" kwa raia wake.

Msimamo huo umetolewa wakati waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas amewasili Israel leo akiwa na ujumbe wa kuiunga mkono nchi hiyo, lakini pia akitoa wito wa kusitishwa mapigano.

Kwenye mkutano na waandishi habari akiwa na mwenzake wa Israel Gabi Ashkenazi, Maas amesema "Nimekuja hapa leo kuwahakikishia mshikamano wetu. Siku za karibuni tumesisitiza na tutaendelea kufanya hivyo siku za usoni kwamba Israel inayo haki ya kujilinda dhidi ya mashambulzii haya makubwa na yasiyokubalika"

Kuna ishara ndogo ya kusitishwa mapigano 

Tangu kuanza kwa mapigano hayo Wapalestina 230 wameuwawa ikiwemo watoto 65 na wanawake 39 na wengine zaidi ya 1,710 wamejeruhiwa. Wapalestina wengine 58,000 wameyahama makaazi yao kukimbia hujuma za ndege za Israel au baada ya nyumba zao kuharibiwa.

Weltspiegel 20.05.2021 | Nahost Gaza / Israel
Picha: IBRAHEEM ABU MUSTAFA/REUTERS

Wapatanishi kutoka Misri nao wanaendelea na juhudi za kusimamisha mapigano na mwanadiplomasia mmoja wa Misri amesema wanasubiri jibu kutoka Israel kuhusu pendekezo la kusitisha mashambulizi.

Afisa wa ngazi ya juu wa kundi la Hamas amesema anatumai mapigano yatasitishwa katika muda wa siku moja au mbili zinazokuja.

Mwandishi: Rashid Chilumba/AP

Mhariri: Grace Patricia Kabogo