1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yakanusha kuvujisha mkutano na waziri wa nje wa Libya

28 Agosti 2023

Wizara ya Nje ya Israel imesema haikuvujisha taarifa za kikao kati ya waziri wake, Eli Cohen, na mwenzake wa Libya, Najla al-Mangoush, ambaye kwa sasa amesimamishwa kazi kufuatia maandamano makubwa nchini mwake.

https://p.dw.com/p/4VfLj
Libyen | Proteste gegen Israel
Picha: Yousef Murad/AP Photo/picture alliance

Hata hivyo, wizara hiyo haikuweka wazi ni nani aliyevujisha habari za kikao hicho kilichotajwa kama hatua ya awali kabisa ya kidiplomasia kati ya Libya na Israel.

Inasemekana mawaziri hao walizungumzia, pamoja na masuala mengine, namna ya kuwa na mahusiano mazuri baina ya mataifa yao.

Soma zaidi: Mwanadiplomasia wa juu Libya asimamishwa kazi baada ya kukutana na mwenzake wa Israel

Israel na Libya hazina mahusiano ya kidiplomasia na kisheria ni kosa kwa afisa ama raia wowote wa Libya kuanzisha mahusiano yoyote na Israel.

Tangazo la mkutano huo liliibua maandamano katika baadhi ya miji ya Libya hatua iliyochochea Mangoush kusimamishwa kazi na Waziri Mkuu Abdulhamid Dbeibah.

Kulingana na shirika la habari la Anadolu la nchini Uturuki, Mangoush tayari ameondoka kuelekea Istanbul kufuatia mzozo huo wa kidiplomasia, ingawa bado hakujatolewa taarifa rasmi.