1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaelezea kuhusu mashambulio nchini Iran

11 Juni 2021

Aliyekuwa mkuu wa Shirika la Ujasusi la Israel Yossi Cohen amekubali kwa kiasi fulani kwamba nchi yake ilihusika katika mashambulio ya hivi karibuni yaliyolenga vinu vya nyuklia vya Iran na mwanasayansi wa kijeshi.

https://p.dw.com/p/3ukJu
Israel Yossi Cohen - Chef des Mossad 2015
Yossi Cohen- Mkuu wa shirika la ujasusi la Mossad anayeondokaPicha: picture-alliance/dpa/O. Messinger

Matamshi ya Cohen pia yalitoa onyo wazi kwa wanasayansi wengine katika mpango wa nyuklia wa Iran kwamba wao pia wanaweza kuwa walengwa wa mauaji,  hata katika wakati ambapo wanadiplomasia wanajaribu kuuokoa Mkataba wa Nyuklia kati ya Iran na mataifa yenye ushawishi duniani. Cohen ameongeza kuwa iwapo kuna mwanasayansi wa Kiirani anataka kubadilisha kazi yake na hatawaathiri tena, wakati mwingine huwa wanampa mwelekeo wa kufuata.

Miongoni mwa mashambulio yanayoilenga Iran, hakuna ambalo limeleta madhara makubwa kuliko miripuko miwili katika kipindi cha mwaka jana katika kinu chake cha nyuklia cha Natanz. Katika kinu hicho, kuna mitambo ya kuimarisha urani kutoka vyumba vya chini ya ardhi vilivyojengwa kuzilinda kutokana na mashambulio ya angani. Mnamo mwezi Julai mwaka 2020, shambulio lisilo la kawaida lilipasua mitambo hiyo ya nyuklia ambapo Iran iliilaumu Israel. Baadaye mwezi Aprili mwaka huu, mripuko mwingine ulibomoa moja ya vyumba vyake vya ardhini vya kuimarisha urani.

Netanjahu scheitert in Israel mit Regierungsbildung
Benjamin Netanyahu - Waziri mkuu wa IsraeliPicha: Yonathan Sindel/UPI Photo/imago images

Wakizungumzia kuhusu Natanz, mwendesha kipindi hicho alimuuliza Cohen ni wapi angewapeleka iwapo wangefanya ziara katika eneo hilo na Cohen akasema ni katika eneo lake la chini ambapo mitambo hiyo ya  nyuklia ilikuwa ikizunguka. Cohen aliongeza kuwa eneo hilo halina muonekano kama ilivyokuwa awali.

Masuala mengine yaliozungumziwa

Pia walijadili mauaji ya Novemba ya Mohsen Fakhrizadeh, mwanasayansi wa Iran ambaye aliasisi mpango wa nyuklia wa Tehran miongo kadhaa iliyopita. Mashirika ya ujasusi ya Marekani na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA, yanaamini kuwa Iran iliachana na juhudi hizo za kutafuta silaha za nyuklia mnamo 2003. Iran kwa muda mrefu imeshikilia kwamba mpango wake ni wa amani.

Mara kwa mara, Iran imelalamika kuhusu mashambulio ya Israeli huku balozi wa Iran katika shirika la IAEA, Kazem Gharibabadi, Alhamisi akionya kuwa visa hivyo havitajibiwa tu kwa kuvimaliza lakini pia hakutakuwa na chaguo kwa Iran ila kufikiria tena hatua zake za uwazi na sera ya ushirikiano. Ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa haukujibu mara moja kuhusu ombi la tamko kuhusu matamshi ya Cohen. Wakati wa mahojiano hayo, Cohen alisema kuwa huenda siku moja akawania wadhifa wa waziri mkuu.