1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaapa kuendeleza mashambulizi Ukanda wa Gaza

14 Desemba 2023

Israel imeazimia kuendelea na mashambulizi katika ukanda wa Gaza hadi itakapoliangamiza kundi la wanamgambo la Hamas katika moja ya mapigano makali zaidi.

https://p.dw.com/p/4a8u4
Israel Tel Aviv |  Benjamin Netanjahu  Waziri Mkuu wa Israel
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akizungumza na waandishi wa habari ambao hawapo kwenye pichaPicha: Xinhua/IMAGO

Israel imeweka wazi hayo  wakati ambapo inakabiliwa na ongezeko la miito ya kimataifa ya kusitishwa kwa mapigano hayo na wasiwasi kwa upande wa mshirika wake wa karibu, Marekani.

Akiwahutubia wanajeshi wake hapo jana kwa njia ya redio, Netanyahu amesema hakuna kitakachoizuia Israelkufikia malengo ya ushindi katika kampeni yake huko Gaza.

Soma pia:Israel imeendelea kukabiliwa na shinikizo la kimataifa yanayotaka isitishe mashambulizi yake kwenye Ukanda wa Gaza

Akiwapa mori ya kuendelea na mapambano katika uwanja wa vita Netanyahu aliwaambia wanajeshi wake kwamba wao ndio sababu ya kufikia malengo ya kampeni hiyo.

"Tunafanya hivyo kwa sababu yenu, kupitia nyinyi, kwa msaada wa Mungu na kwa msaada wenu. Asanteni sana." Alisema Waziri Mkuu huyo.

Haya yanajiri wakati ambapo mshauri wa usalama wa kitaifa wa Marekani  Jake Sullivan anatarajiwa kufanya ziara nchini Israel leo. 

Marekani imeishinikiza Israel kuchukua hatua zaidi kuwalinda raia, na mapema wiki hii, Rais wa nchi hiyo Joe Biden, alisema kwamba Israel inapoteza uungwaji mkono wa kimataifa kwa sababu ya mashambulizi yake ya mabomu aliyoyaita kuwa '' Ya kiholea''