1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita ya Israel Gaza yaigharimu katika bajeti yake

8 Novemba 2023

Wizara ya Fedha ya Israel imesema hii leo kuwa na nakisi ya dola bilioni 6 katika bajeti yake kutokana na kuongezeka kwa gharama za kufadhili vita vyake dhidi ya wanamgambo wa Hamas katika ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4YaNV
Waziri wa Mambo ya nje wa Israel Eli Cohen
Waziri wa Mambo ya nje wa Israel Eli CohenPicha: Shannon Stapleton/REUTERS

Wizara hiyo imebaini kuwa mapato ya taifa hilo yalipungua kwa asilimia 15.2 mwezi uliopita kutokana na ucheleweshaji wa kodi na kupungua kwa mapato ya mfumo wa ustawi wa jamii kutokana na vita vilivyoanza Oktoba 7 mwaka huu. 

Hayo yanajiri wakatimapigano makali yakiendelea kuripotiwa huko Gaza ambako kwa sasa idadi ya vifo imefikia takriban watu 10,500 kwa mujibu wa wiraza ya Afya inayodhibitiwa na kundi la Hamas. 

Soma pia:Israel yaendelea kuishambulia Gaza angani na ardhini

Akiwahutubia wabunge wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji hii leo, Waziri wa Mambo ya nje wa Israel Eli Cohen amesema vita vya Israel vya kuiangamiza Hamas huko Gaza ni "vita vya ulimwengu huru", na kwamba Israel ilishambulia sio tu Hamas bali na wanamgambo wengine katika eneo hilo wanaoungwa mkono na Iran, ambayo ameitaja kuwa "mfadhili nambari moja wa ugaidi duniani".