1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel inaendeleza mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza

7 Julai 2024

Israel imeendeleza mashambulizi yake ya angani katika ukanda wa Gaza, wakati vita kati yake na wanamgambo wa Hamas vikiingia mwezi wake wa kumi.

https://p.dw.com/p/4hymO
Mgogoro wa Mashariki ya Kati
Israel yaendeleza mashambulizi yake katika Ukanda wa GazaPicha: Bashar Taleb/AFP

Israel imeendeleza mashambulizi yake ya angani katika ukanda wa Gaza,  wakati vita kati yake na wanamgambo wa Hamas vikiingia mwezi wake wa kumi. Mapigano yanazidi kote katika maeneo ya wapalestina huku jitihada za kidiplomasia za kujaribu kusitisha mapigano zikiendelea.

Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina limesema mashambulizi ya leo, yamesababisha mauaji ya watu sita wakiwemo watoto wawili ambao miili yao imepelekwa katika hospitali ya Al Aqsa, iliyoko mjini Deir al Balah. 

Kundi la Hamas lafahamisha Hezbollah kuwa limekubali kusitisha mapigano Gaza.

Hapo Jana wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas ilisema watu 16 waliuwawa katika shambulizi lililofanywa dhidi ya shule moja, inayoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi Wakipalestina UNRWA.

Kando na hayo Israel imesema itatuma wajumbe wake ndani ya siku kadhaa zijazo kuendelea na mazungumzo yaliyoanzishwa hivi karibuni na wapatanishi wa Qatar ya kusitisha mapigano yanayoendelea Gaza. Lakini Waziri Mkuu Bemnjamin Netanyahu amesema Hamas ndio wanaotarajiwa kujaza pengo katika mazungumzo hayo ya kuamua ni vipi watakavyojitolea kikamilifu kusitisha vita na kuwaachia mateka inaowashikilia.