1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Isaac Herzog achaguliwa rais mpya wa Israel

Sylvia Mwehozi
2 Juni 2021

Bunge la Israel limemchagua kiongozi wa zamani wa upinzani Isaac Herzog kuwa rais mpya wa nchi hiyo na atachukua mikoba ya rais anayemaliza muda wake Reuvin Rivlin mnamo Julai 9

https://p.dw.com/p/3uMH0
Israel neu gewählter Präsident Izchak Herzog
Picha: Manuel Balce Ceneta/AP/dpa/picture alliance

Kiongozi huyo wa zamani wa upinzani mwenye umri wa miaka 60 amechaguliwa kwa kura 87 za ndiyo dhidi ya 26 za hapana na kumshinda mpinzani wake mwanaharakati na mwalimu Miriam Peretz.

Herzog alitangaza kwamba atakuwa "rais wa Waisrael wote" na kufanya kazi kuelekea katika kuliunganisha taifa hilo lililogawika. "Sasa ni muda wa kujenga madaraja", alisema Herzog akiongeza kwamba atapambana dhidi ya chuki ya Waisrael kote ulimwenguni.

"Nadhamiria kuwa rais wa kila mmoja, kusikiliza kila upande wa kisiasa, kumheshimu kila mtu, kuashiria kile kinachotuunganisha pamoja na kujenga madaraja ya makubalino."

Kiongozi huyo aliwahi kuchuana na waziri mkuu Benjamin Netanyahu katika uchaguzi wa bunge wa 2015.

Rais mteule wa Israel na spika wa bunge Yariv Levin(kulia)
Rais mteule wa Israel na spika wa bunge Yariv Levin(kulia)Picha: Ronen Zvulun/Reuters/AP/picture alliance

Herzog alizaliwa mjini Tel Aviv na kwa muda mrefu amekuwa katika ulingo wa siasa. Alikiongoza chama cha Labour tangu mwaka 2013. Anatoka katika familia kubwa ya kizayuni na baba yake Chaim Herzog alikuwa balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa kabla ya kuchaguliwa kuwa rais kati ya mwaka 1983-93.

Herzog atakuwa rais wa 11 akimrithi Rivlin, ambaye ataondoka ofisini mwezi ujao baada ya kukaa mamlakani kwa miaka saba. Mjomba wake Abba Eban alikuwa waziri wa mambo ya nje wa Israel na balozi katika Umoja wa Mataifa na Marekani.

Babu yake alikuwa ni kiongozi wa juu wa kwanza wa kidini nchini Israel. Herzog amemshinda Miriam Peretz mwenye umri wa miaka 67 ambaye kitaaluma ni mwalimu na aliyeonekana kuwa karibu na wahafidhina na kambi ya kitaifa ya kisiasa.Likud na Labour kuunda serikali Israel?

Herzog pia aliwahi kuwa mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Israel linalohamasisha uhamiaji nchini humo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita tangu alipojiuzulu bungeni. Kwa kawaida rais wa Israel anakuwa na jukumu la kumpa idhini kiongozi wa chama cha kisiasa kuunda serikali.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amempongeza Herzog kupitia ukurasa wa Twitter akimtakia kila lenye heri katika majukumu yake mapya.

Wakati huo huo wapinzani wa Netanyahu wanakabiliwa na muda wa mwisho wa usiku wa Jumatano wa kuunda serikali ya mseto. Kama watashindwa, nchi hiyo inaweza kutumbukia katika dimbwi jingine la uchaguzi.