1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IS wawauwa askari 40 wa zamani wa Iraqi

1 Novemba 2016

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu, IS, jumamosi iliyopita wamewauwa askari wa zamani wa vikosi vya usalama vya Iraqi wapatao 40, katika eneo karibu na mji wa Mosul na kutupa miili yaao katika mto Tigris.

https://p.dw.com/p/2RzUo
Ravina Shamdasani , Sprecherin UNHCR
Picha: UNHCR Presse Büro

Msemaji wa masuala ya haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani, Jumanne hii (01.11.2016) ametoa taarifa hiyo, akiangazia ripoti kutoka eneo lilipotokea tukio hilo. 

Taarifa kutoka Umoja wa Mataifa, Geneva zinaeleza kwamba kundi hilo la Dola la Kiislamu pia lilijaribu kuwasafirisha raia 25,000 kutoka Hammam al-Alil, mji ulioko Kusini mwa Mosul, wakiwa kwenye malori na mabasi madogo wakati kulipoanza kuingia giza, mnamo siku ya jumatatu, na lengo lao likidhaniwa kuwa ni kuendelea kuwatumia raia hao kama ngao ya vita kwenye maeneo yao yanayolengwa na majeshi, Shamdasani amesema.

Amesema, hatua hiyo moja kwa moja inadhihirisha kwamba wanataka kuwatumia raia hao kama ngao ya vita, pamoja na kujihakikishia kwamba eneo lao linakuwa na raia wengi ili kuyafanyia ugumu majeshi ya usalama katika operesheni yake ya kuwafurusha na kuukomboa mji wa Mosul. Wamekuwa pia wakiwauwa baadhi ya watu waliowateka, hususan wale waliowahi kuwa askari wa jeshi la Iraqi.

Askari hao 40 wa zamani waliouwawa Jumamosi iliyopita walikuwa ni kati ya raia waliowateka mapema katika wilaya ndogo ya Mosul, al-Shura, pamoja na vijiji vingine vinavyozunguka Hamman´m al-Alil. 

Kwingineko huko Iraqi, inaarifiwa kuwa vikosi vya usalama va Iraqi vimeingia kwenye viunga vya Mosul, na kulikamata jengo lenye  kituo cha televisheni cha Mosul, kama sehemu ya mashambulizi hayo ya kuwaondoa wapiganaji wa Dola la Kiislamu kutoka kwenye mji huo, chanzo cha habari cha jeshi kimesema. 

Irak Kämpfe in Qaraqosh
Askari wa Iraqi akipita katika viunga vya mji wa Qaraqosh, wakati vikosi vya serikali vilipokuwa vikiwasaka wapiganaji wa IS.Picha: REUTERS/A. Jadallah

Kiongozi wa vikosi vya kukabiliana na ugaidi vya nchini Iraqi Taleb Shaghti amekiambia kituo cha televisheni cha serikali al-Iraqia kwamba vikosi vyake vimefika katika kituo cha mwisho cha Bazwaya, panapokaliwa na watu wengi masikini, eneo ambalo lilikombolewa jana jumatatu. "Hii inamaanisha kuwa tumeanza ukombozi kamili wa Mosul kwa sababu tumekwishaingia kwenye mpaka wa kiutawala wa ecityu" amesema.

Meja Generali wa vikosi maalumu kwenye mashambulizi ya kuukomboa mji wa Mosul, Sami al-Aridi amesema askari wake wameingia kwenye viunga vya Mosul na walikuwa wakisonga mbele, pamoja na kukabiliwa na mashambulizi kutoka kwa wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu wanaoushikilia mji huo.

Majeshi ya Iraqi, yamekabiliana kwa risasi na wapiganaji wa IS katika eneo lenye viwanda lililopo Gogjali, karibu na lango kuu  linaloingia wilaya ya kwanza ya Mji wa Mosul, Mashariki mwa mji huo, tovuti ya masuala ya habari ya Rudaw imeripoti. Wapiganaji wa IS, wametumia wataalamu wa kulenga na mabomu ya kutengeneza kuyasimamisha majeshi hayo.

Majeshi hayo ya usalama, kwa kushirikiana na vikosi vya wapiganaji wa Kikurdi na kutoka madehebu ya Sunni na yanayoungwa mkono na muungano wa majeshi unaoongozwa na Marekani kwa pamoja walianzisha mashambulizi hayo dhidi ya IS ya kuukomboa mji wa Mosul, ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Iraqi.

Mwandishi: Lilian Mtono/eap/dpae/afpe.
Mhariri: Yusuf Saumu