1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yathibitisha vifo vya kwanza vya virusi vya Corona

Sylvia Mwehozi
20 Februari 2020

Iran imethibitisha vifo vya watu wawili vilivyotokana na maambukizi mapya ya virusi vya Corona na kuvifanya kuwa vifo vya kwanza kuripotiwa eneo la Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/3Y2OV
Südkorea Daegu | Coronavirus | mutmaßlicher Patient
Picha: picture-alliance/dpa/YNA

Nchini China maambukizi yanaendelea kupungua ingawa wataalamu wanaonya kwamba virusi hivyo vinaweza kuenea zaidi kuliko ilivyodhaniwa. Maafisa wa afya nchini Iran, walithibitisha visa viwili vya maambukizi mapya ya virusi vya Corona vilivyopewa jina la COVID-19 ambapo wanaume wawili wazee wamepoteza maisha katika mji wa Qom. Shirika la habari la Iran IRNA, limesema shule na vyuo huenda vikafungwa katika mji huo wa Qom kwa ajili ya kufanya uchunguzi.

Iran imeanza kuchukua hatua za tahadhari hususan katika viwanja vya ndege ambapo abiria tofauti wanawasili. Vifo hivyo ni vya kwanza kuripotiwa katika eneo la Mashariki ya kati. Kwingineko watu tisa wameripotiwa kuwa na maambukizi ya Corona katika nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

China imeripoti kuendelea kupungua kwa kasi ya maambukizi na kuweka matumaini ya kumalizika kwa mripuko huo, huku Japan ikikoselewa kutokana na abiria wawili waliokuwamo ndani ya meli iliyowekwa chini ya karantini kupoteza maisha.

Idadi ya vifo ndani ya China bara imefikia watu 2,118 baada ya watu wengine 114 kufariki, lakini maafisa wa afya wameelezea kiwango kidogo cha maambukizi mapya kulinganisha na hapo awali. Zaidi ya watu 74,000 wameambukizwa virusi hivyo ndani ya China na mamia wengine katika nchi zaidi ya 25.

Coronavirus - Japan - Diamond Princess Kreuzfahrtschiff
Mabasi yaliyowabeba abiria walioondolewa kwenye meli ya Diamond Picha: picture-alliance/dpa/AP/E. Hoshiko

Wakati China ikishuhudia kupungua kwa maambukizi ya mripuko wa COVID-19, serikali ya Japan imekabiliwa na ukosoaji juu ya hatua za kuiweka chini ya karantini meli ya Diamond Princess. Michael Ryan ni mkurugenzi wa huduma za dharura kutoka WHO na anasema.

"Ni dhahiri kwamba mamlaka za Japani awali zilifanya uamuzi wa kuwaweka karantini abiria wote kwenye meli hiyo, ambapo abiria waliwekwa pamoja katika mazingira ambayo wanaweza kufuatiliwa na kupatiwa makazi tofauti na kila kitu kingine".

Siku ya Jumatano karibu abiria 500 waliondolewa ndani ya meli hiyo baada ya kubainika kutokuwa na maambuki ya corona. Abiria zaidi wameondoka ndani ya meli hiyo leo Alhamis.

Wakati huo huo wanasayansi wa China wanazijaribu dawa mbili za kupambana na virusi hivyo na matokeo ya awali yatatolewa wiki zinazofuata. Daktari Marie-Paule Kieny ambaye ni mtaalamu wa zamani wa maradhi ya mripuko kutoka shirika la afya ulimwenguni WHO, aliendesha utafiti wa siku mbili mjini Geneva wa wanasayansi zaidi ya 300 na watafiti, wakiwemo kutoka China na Taiwan.

Dr. Kieny amesema kuwa "bado haijafahamika ikiwa tiba hiyo itathibitisha ufanisi dhidi ya virusi vipya" na kwamba hawajui matokeo hivyo wanapaswa kusubiri kwa siku kadhaa. Korea Kusini nayo imeripoti maambukizi mapya 31 ya Corona na kufanya idadi ya walioambukizwa kufikia 82.

Vyanzo: afp/reuters/ap