1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yatakiwa kufuata maagizo ya Umoja wa mataifa juu ya mpango wake wa Kinuklia

31 Machi 2006

Mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa yenye nguvu walikutana mjini Berlin na kujadili mikakati ya hatua zakuchukua endapo Iran haitofuata maagizo.

https://p.dw.com/p/CBJC
Mawaziri wa mambo ya nje waliokutana kujadadili suala la mpango wa Kinuklia wa Iran,mjini Berlin
Mawaziri wa mambo ya nje waliokutana kujadadili suala la mpango wa Kinuklia wa Iran,mjini BerlinPicha: AP

Mkutano huu wa mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi tano wanachama wa kudumu kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani,umekuja siku moja baada ya baraza hilo kupitisha kauli ya kuitaka Iran ikomeshe shughuli zake za kurutubisha madini ya Uranium.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condolezza Rice ametaka kuwepo na mikakati ya muda mrefu kuzuia mpango wa kinuklia wa Iran unaotiliwa shaka.

Kauli hiyo imelitaka shirika la kimataifa la kudhibiti technologia ya Nukilia IAEA kuripoti kwa baraza hilo baada ya muda wa siku 30 juu ya iwapo Iran imetekeleza matakwa hayo ya kusitisha mipango yake ya kurutubisha Uranium au la.

Tayari Iran imesema hii leo kwamba haitopangua mpango wake wa Kinuklia kutokana na kauli hiyo ya Umoja wa mataifa ya kuitaka Iran iuonyeshe ulimwengu kwamba mpango wake wa Kinuklia ni wa amani.

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa Javad Zarif anasema Iran imeshaweka wazi kwamba mpango wake ni kwa ajili ya matumizi ya amani,anasema.

„Marekani tangu mwanzo ilitaka mazungumzo hayo yasifanikiwe.Madhumuni tangu mwanzo yalikuwa ni kuifikisha Iran mbele ya baraza löa usalama la Umoja wa Matafaifa.

Iran haikubaliani na shinikizo na wala hatukubali vitisho.

Akizungumza na shirika la habari la Reuters balozi wa Iran kwenye shirika la kimataifa la kudhibiti tecnologia ya Kinuklia IAEA;Aliasghar Solataniyeh amesema Iran katu haiwezi kusimamisha tena mpango wake wa Kinuklia.

Iran imetoa msimamo wake huo wakati mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani,Uingereza,Ufaransa,China,Urusi na Marekani wanajadili juu ya hatua watakazochukua endapo Iran haitotekeleza matakwa yaliyotolewa na baraza la usalama katika muda wa siku 30.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Manoucher Mottaki ameitaja hatua ya baraza la usalama ya kupitisha kauli kuitaka iran isimamishe mpango wake wa Nuklia kuwa mbaya.Anasema

Tunaamini uamuzi kuhusu mpango wa Nuklia wa Iran uliochukuliwa na baraza la usalama ni hatua iliyochochewa kisiasa.

Hatua hii imeifanya umuhimu wa baraza la usalama kuwa dhaifu.

Hatua hii baadae itadhoofisha msimamo wa shirika la kimataifa la kudhibiti tecnologia ya kinuklia IAEA.

Suala la mpango wa Nuklia ya Iran linabidi kujadiliwa na shirika la IAEA:

Hatua ya kulifikisha suala la Iran mbele ya Baraza la usalama la Umoja wa mataifa kwa sababu tu ya Iran kurutubisha madini yake ya Uranium ni makosa.

Bwana Mottaki badala yake anasema serikali ya Tehran iko tayari kuendelea na mazungumzo na kwamba wapo wazi kwa mashauriano yoyote yanayoihakikishia haki ya taifa la Iran.

China kwa upande mwingine hata hivyo imesema bado kuna muda wa kuutatua mzozo huo wa kinuklia wa Iran kidiplomasia.