Iran yataka mazungumzo ya amani ya Yemen
9 Aprili 2015Rais Hassan Rouhani wa Iran ametoa wito wa kufikishwa mwisho kwa mashambulizi ya angani yanayofanywa na Saudi Arabia na washirika wake wa mataifa ya Kiarabu, kwa kusema hayawezi kufanikiwa na hivyo kuyataka mataifa katika kanda hiyo kutafuta suluhu kwa mwelekeo kisiasa.
Katika hotuba yake kupitia televisheni rais Rouhani alisema kwa mtazamo wake taifa kama Yemen haliwezi kusalimu amri kwa sababu ya mabomu na kuongeza kwamba wote waje pamoja na kufikiria namna ya kumaliza vita. Wanapaswa kufikiri kuhusu kusitishwa mapigano.
Wiki mbili za mashambulizi
Saudi Arabia na muungano wa majeshi wenye kujumuisha mataifa ya Ghuba ya Uarabuni yameendesha mashambulizi ya angani dhidi ya harakati za Houthi katika kipindi cha takribani wiki mbili kwa lengo la kuwaondoa wapiganaji hao katika mji wa kusini wa Aden.
Muungano huo unasema unamuunga mkono rais wa Yemen Abdi-Rabbu Mansour Hadi dhidi ya jaribio la mapinduzi la Houthi na vilevile kuituhumu Iran kwa kulipa silaha kundi hilo, madai ambayo yamekanushwa na taifa hilo linalofuata madhehebu ya Kiislamu ya Shia.
Marekani yaionya Irani
Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry amesema taifa lake haliwezi kujiweka kando wakati Iran ikiwasaidia waasi wa Kishia ambao wameyateka maeneo mengi ya Yemen. Waziri Kerry alikiambia kituo cha televisheni cha PBS kwamba wamebaini kuwa kila baada ya wiki kumekuwa na ndege za Iran zinazotua katika ardhi ya Yemen.
Kutokana na kitendo hicho amesema Iran lazima itambue kwamba Marekani haiwezi kukaa kimya wakati hali ya utulivu ikivurugwa katika kanda hiyo.
Marekani inaunga mkono muungano wa mataifa yenye idadi kubwa ya Waislamu wa Madhehebu ya Sunni, wenye kuongozwa na Saudi Arabia, ambao unaendesha kampeni ya mashambulizi ya angani katika jitihada zake za kumrejesha madarakani Rais Abdi-Rabbu Mansour Hadi wa Yemen ambae amelazimishwa kulikimbia taifa lake.
Waasi 20 wauwawa katika mapigano
Na katika uwanja wa mapambano kiasi ya waasi 20 wa Houthi wameuwawa huko kusini mwa Yemen, kufuatia mashambulizi ya anga ya muungano unaongozwa na Saudi Arabia pamoja na kukabiliwa vikali na wapiganaji wanaounga mkono serikali. Chanzo kimoja kutoka kwa wapiganaji hao kilisema wapiganaji 14 wa Houthi waliuwawa katika mashambulizi hayo karibu na wilaya ya Dar Saad, iliyopo kusini mwa Aden. Na wengine sita wameuliwa na wanapiganaji watiifu kwa serikali katika karibu na mji wa Daleh.
Waasi wa Houthi wamefanikiwa kudhibiti sehemu kubwa ya Yemen, ikiwemo mji mkuu wa Sanaa, na kuungana na wapiganaji watiifu kwa mtawala wa zamani wa muda mrefu wa taifa hilo Ali Abdullah Saleh, ambae alilazimishwa kuondoka madarakani mwaka 2012 baada ya mwaka mmoja tangu kuanza kwa vuguvugu la mataifa ya Kiarabu.
Mwandishi: Sudi Mnette AFP RTRE
Mhariri: Iddi Ssessanga