1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali Yemen yatajwa ya maangamizi

8 Aprili 2015

Shirika la msalaba mwekundu limeonya hali ni ya maangamizi katika mji wa kusini mwa Yemen wa Aden huku majeshi yanayomuunga mkono Rais wa Yemen Abedrabbo Mansour Hadi yakipambana na waasi wa Houthi katika mji huo.

https://p.dw.com/p/1F3yg
Picha: picture-alliance/dpa

Waasi wa kishia wa kundi la Houthi wamejaribu kueneza mashambulizi yao katika eneo la Muallah mjini Aden wakipania kuudhibiti mji huo lakini wamekabiliwa na mashambulizi makali kutoka kwa wanajeshi na wapiganaji wanaomuunga mkono Rais wa Yemen aliyetorokea Saudi Arabia Abedrabbo Mansour Hadi.

Walioshuhudia mapigano hayo wamesema majeshi ya majini ya Saudi Arabia ambayo inaongoza kampeini ya mashambulizi ya angani dhidi ya wahouthi kwa wiki mbili sasa, yameyashambulia maeneo ya waasi hao mjini Aden lakini muungano huo wa nchi za kiarabu na za ghuba umekanusha kufanya operesheni kwa kutumia majeshi ya majini.

Hali ni ngumu mno kote Yemen

Msemaji wa shirika la kimataifa la msalaba mwekundu Marie Claire Feghali amesema hali ni ngumu mno kote nchini Yemen kutokana na mashambulizi ya angani, majini na ya nchi kavu ambayo yamekatisha njia zote za kuwasilisha misaada ya kibinadamu inayohitajika kwa dharura.

Familia moja ya Yemen ikiyatoroka mapigano mjini Sanaa
Familia moja ya Yemen ikiyatoroka mapigano mjini SanaaPicha: Reuters/K. Abdullah

Hata hivyo Jenerali Ahmed Assiri wa Saudi Arabia anayeongoza kampeini ya kijeshi amekanusha madai hayo ya shirika la msalaba mwekundu na kusema maeneo mengi mjini Aden yako salama. Shirika la kimataifa la madaktari wasio na mipaka la MSF limesema hali inazidi kuwa mbaya kila uchao.

Assiri amesema kibali kimetolewa kwa misaada ya vifaa na wahudumu wa matibabu kufikishwa nchini humo kutoka Djibouti na shirika la msalaba mwekundu limesema linatumai kuwasiliha tani 16 za misaada ya vifaa vya matibabu mjini Sanaa hii leo kwa ndege kutoka Jordan.

Shirika la afya duniani limesema zaidi ya watu 560 wameuwa nchini Yemen, katika kipindi cha wiki mbili zilizopita wengine zaidi ya 1,700 wamejeruhiwa na maelfu kuachwa bila ya makaazi huku umoja wa Mataifa ukisema unahofia idadi ya waathiriwa ni kubwa hata kuliko hiyo.

Marekani yatiwa wasiwasi

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Ashton Carter ametangaza kuwa wanaharakisha kutuma silaha kuunga mkono kampeini ya kijeshi inayoongozwa na Saudi Arabia huku akionya kuwa wanamgambo wenye itikadi kali wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda huenda wakachukua fursa ya kuwepo msukosuko Yemen kueneza ngome zao nchini humo.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton Carter
Waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton CarterPicha: AFP/Getty Images/N. Kamm

Nchi za kiarabu pia zinalitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwaweka katika orodha ya watu wa kuwekewa vikwazo mwana wa kiume wa Rais wa zamani wa Yemen Ahmed Saleh na kiongozi wa kundi la waasi la Houthi Abdulmalik Houthi.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif ambaye nchi yake inashutumiwa kwa kuuchochea mzozo wa Yemen anatarajiwa kufanya mazungumzo hii leo na viongozi wa Pakistan mjini Islamabad kuhusu hali hiyo ya Yemen.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/Afp

Mhariri: Hamidou Oummilkheir