1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiIran

Kiongozi wa mtandao wa kuwasafirisha wanawake anyongwa Iran

20 Mei 2023

Iran imesema leo kuwa imemnyonga kiongozi wa mtandao mkubwa uliokuwa ukiwasafirisha wanawake wa nchi hiyo kwenda mataifa jirani kufanya shughuli za ukahaba.

https://p.dw.com/p/4RbVe
Kitanzi hutumika kutekeleza adhabu ya kifo nchini Iran
Kitanzi hutumika kutekeleza adhabu ya kifo nchini Iran Picha: Allison Bailey/NurPhoto/picture alliance

Mahakama ya taifa hilo imesema Sharooz Sakhnoori, mwanaume aliyekuwa akifahamika pia kwa jina la "Alex" amenyongwa asubuhi ya leo baada ya kukutwa na hatia ya kuongoza genge la kuwaingiza wanawake na wasichana wa Iran kwenye ukahaba.

Mwanaume huyo alikamatwa nchini Malasyia mnamo mwaka 2020 kwa ushirikiano kati ya Iran na polisi ya kimataifa, Interpol. Inaarifiwa aliondoka nchini Iran mwaka 1983 na kuishi kwenye mataifa kadhaa ikiwemo India, Malaysia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Marekani.

Iran ni miongoni mwa mataifa yenye sheria kali za kulinda maadili, lakini imelaumiwa miaka ya karibuni kwa kushindwa kuzuia biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.