1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yakaribisha mazungumzo na Saudi Arabia

19 Aprili 2021

Msemaji wa Wizara ya mambo ya kigeni wa Iran amesema taifa hilo siku zote limekuwa likiyakaribisha mazungumzo na mpinzani wake wa kikanda Saudi Arabia, kwa nia ya kuwa na amani na uthabiti wa eneo zima.

https://p.dw.com/p/3sEUe
Iran Außenpolitischer Sprecher Saeed Khatibzadeh
Picha: Fatemeh Bahrami/AA/picture alliance

Mataifa hayo mawili Iran na Saudi Arabia yalikatisha mahusiano yao mwaka 2016 na yamekuwa yakipigana vita vya uwakala, wote waking'ang'ania kuwa na ushawishi wa kikanda. Uhasama kati yao uliongezeka mwaka 2019 baada ya misururu ya mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya vituo vya mafuta vya Saudi Arabia. Marekani iliishutumu Iran kwa matukio hayo jambo ambalo Iran imeendelea kukanusha.    

Afisa mmoja wa Iran na duru mbili za habari kwenye kanda hiyo zimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba maafisa wa mataifa hayo mawili walikutana kwa mazungumzo nchini Iraq tarehe 9 Aprili katika kile kinachosemekana kuwa ni hatua ya kutuliza mvutano kati yao wakati Marekani ikiwa mbioni kujaribu kuyafufua makubaliano ya nyuklia ya Iran ya mwaka 2015 pamoja na kumaliza vita vya Yemen.

soma zaidi:  Hofu yazuka baada ya Iran kurutubisha madini ya urani

Gazeti la Financial Times liliripoti kufanyika kwa mkutano huo.  Lakini Msemaji wa wizara ya kigeni ya Iran Saeed Khatibzadeh hakukubali wala kukataa kufanyika kwa mkutano huo, ila amesema kilicho muhimu kwa sasa ni kwamba Iran imekuwa tayari siku zote kuwa na mazungumzo na Saudi Arabia, mazungumzo yalio na lengo la kuwa na uthabiti na amani ya kikanda.

Mazungumzo yanadaiwa kugusia Mkataba wa nyuklia wa Iran na vita vya Yemen

Jemen Sanaa | Bewaffnete Houthi Anhänger
Waasi wa Houthi walioungwa mkono na Iran Picha: Khaled Abdullah/REUTERS

Saudi Arabia bado haijaitikia ombi la Reuters kuzungumzia mkutano huo wa awali kati yake na Iran lakini Afisa mmoja ambaye hakutaka kutambulishwa amesema mkutano huo ulioandaliwa na Waziri Mkuu wa Iraq aliyeitembelea Saudi Arabia mapema mwezi huu ulijadili hali ilivyo nchini Yemen ambako muungano wa kijeshi unaoongozwa na Riyadh umekuwa ukipambana na waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Tehran.

Haya yanaripotiwa wakati mazungumzo ya Vienna yaliyoijumuisha Iran na mataifa yaliyo na nguvu duniani, yakijaribu kuirejesha Marekani katika mkataba wa nyuklia wa Iran uliotiwa saini mwaka 2015.

Soma zaidi:  Mazungumzo ya kufufua mkataba wa nyuklia na Iran yafanyika Vienna

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump aliiondoa nchi hiyo katika mkataba wa nyuklia ambao Iran mara kwa mara umeukiuka baada ya Trump kuiwekea vikwazo zaidi vya kiuchumi kwa madai ya Iran kutojitolea kikamilifu kuachana na mipango yake ya kutengeneza silaha za nyuklia.

Awali serikali ya kishia ya Iran imekuwa ikipuuzilia mbali miito inayotolewa na serikali ya Kisunni ya Saudi Arabia kutaka kujumuishwa katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran lakini imezungumzia utayari wake wa kuwa na majadiliano ya kikanda.

Chanzo: reuters/afp/ap