1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Iran yakanusha urutubishaji wa vinu vyake

24 Februari 2023

Televisheni ya kitaifa ya Iran Ijumaa imeitetea serikali ya nchi hiyo kuhusiana na madai yaliyotolewa na wachunguzi wa kimataifa kwamba ilirutubisha madini ya urani hadi asilimia 84 katika vinu vyake vya nyuklia.

https://p.dw.com/p/4Nwnq
Iran Uran l Gebäude des Reaktors des Kernkraftwerks Bushehr
Picha: Behrouz Mehri/AFP

Afisa mmoja wa serikali ya Iran amesema hiyo ni sehemu ya "njama" dhidi ya Iran wakati ambapo kuna mivutano kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Matamshi hayo yaliyotolewa na Behrouz Kamalvandi, msemaji wa mpango wa kiraia wa nyuklia wa Iran yalikuwa yanalenga kuonyesha kwamba ugunduzi wa aina yoyote wa madini ya urani yaliyorutubishwa kwa kiasi hicho, umetokana na kujaribu kufikia asilimia 60 ambayo Iran tayari imetangaza kwamba inarutubisha.

Iran I Techniker arbeiten in der Anlage des Schwerwasserreaktors Arak
Kinu cha nyuklia nchini IranPicha: Atomic Energy Organization of Iran/AP/picture alliance

Lakini madini ya urani yanapofikia asilimia 84 yanakuwa yanakaribia kiwango cha silaha ambacho ni asilimia 90 na hii ina maana kwamba, hifadhi yoyote ya madini hayo yanaweza kutumiwa kutengeneza bomu la atomiki iwapo Iran itaamua kufanya hivyo.

Mvutano kati ya Iran na Magharibi kuzidi

Iran imekuwa ikisisitiza kwamba mpango wake wa nyuklia ni kwa sababu za amani, ingawa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki IAEA, mashirika ya kijasusi ya Magharibi na wataalam wanasema Iran ilikuwa na mpango wa siri wa nyuklia hadi mwaka 2003.

Madai kwamba maafisa wa IAEA wamegundua urutubishaji wa madini ya urani kwa asilimia 84 ni jambo ambalo litazidisha mivutano kati ya Iran na nchi za Magharibi. Tayari Waziri Mkuu mpya wa Israel Benjamin Netanyahu ametishia kuichukulia Iran hatua za kijeshi.

Mkataba wa nyuklia wa Iran wa mwaka 2015, uliiwekea Iran kiwango cha urutubishaji cha hadi asilimia 3.67 ambacho kinatosha kuendesha kiwanda cha nyuklia. Marekani ilijiondoa kutoka kwenye mkataba huo mwaka 2018 na tangu wakati huo, kumeibuka mizozo kati ya Israel na Iran ingawa Marekani haihusiki moja kwa moja katika mzozo huo.

General of the International Atomic Energy Agency (IAEA), Rafael Mariano Grossi
Mkuu wa IAEA Rafael GrossiPicha: Nacho Doce/REUTERS

Iran ina madini ya kutosha kutengeneza mabomu ya nyuklia

Mkurugenzi mkuu wa IAEA ameonya kwamba Iran sasa ina madini ya kutosha ya urani kutengeneza mabomu kadhaa ya nyuklia iwapo itaamua kufanya hivyo, huenda ikachukua miezi kadhaa zaidi kutengeneza silaha na kuiwekea kombora.

Mnamo mwezi Machi mwaka jana, idara ya ujasusi ya Marekani ilisema kwamba Iran haifanyi shughuli zozote kuu za kutengeneza silaha ya nyuklia.

Chanzo: Reuters