1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran imekataa pendekezo la Umoja wa Mataifa

Lillian Urio12 Agosti 2005

Baraza la viongozi wa shirika la masuala ya kinuklia la Umoja wa Mataifa jana lilipitisha pendekezo linalotaka Iran isitishe mara moja mpango wake wa kutengeneza nuklia. Pendekezo hilo limetolewa na mataifa ya Ulaya.

https://p.dw.com/p/CHfK

Iran iliamua kuendelea na mpango wa kutengeneza nuklia mwanzoni mwa wiki hii, baada ya kuusimamisha mpango huo mwezi Novemba mwaka jana.

Pendekezo hilo linataka nchi hiyo kuacha kazi zote zinazohusiana na utengenezaji wa nuklia na pia linataka shirika la masuala ya kinuklia la Umoja wa Mataifa lifuatilie na kuhakikisha iwapo Iran imetekeleza wito huo.

Baadhi ya mataifa ya magharibi, hasa Marekani, yamelalamika kuwa Iran inataka kuwa na silaha za kinuklia. Wakati Iran inapinga na kusisitiza inataka kutengeneza mitambo ya kutengenezea nishati.

Akizungumza na wandishi wa habari msemaji wa shirika la masuala ya kinuklia la Umoja wa Mataifa, Bi. Melissa Fleming, amesema pendekezo hilo lilipitishwa bila kipingamizi kutoka mwakilishi wowote kwenye baraza hilo.

Naye Rais wa marekani, George W. Bush, akizungumza na wandishi wa habari akiwa nyumbani kwake kwenye jimbo la Texas, amesema pendekezo hilo dhidi ya Iran ni uamuzi mzuri. Ameongeza kwamba mpango wa Marekani juu ya suala hili ni kushirikiana na Ujerumani, Uingereza na Ufaransa katika kuishawishi nchi hiyo iache kutaka kuwa na silaha za kinuklia.

Baraza la uongozi la shirika la masuala ya kinuklia la Umoja wa Mataifa lilianza mkutano wake Jumanne iliyopita. Lakini lilikatisha mkutano wao ili kuwapa muda wa kujadili wawakilishi wa Umoja wa Ulaya,juu ya pendekezo hilo na viongozi wa baraza hilo.

Mkutano uliendelea jana na ndipo walipopitisha pendekezo hilo, baada ya majadiliano mengi kufanyika juu ya jinsi lilivyotungwa.

Pendekezo hilo limetayarishwa na Uingereza, Ujerumani na Ufaransa na linataka kiongozi wa shirika la masuala ya kinuklia la Umoja wa Mataifa, Bwana Mohamed Elbaradei, kutayarisha ripoti ya Iran na kama wanafuatilia makubaliano ya mkataba wa kutoendelea kutengeneza silaha za kinuklia.

Pia linasema kwamba Bwana Elbaradei anatakiwa kufuatilia iwapo Iran inatekeleza matakwa ya pendekezo hilo na awasilishe ripoti yake tarehe 3 mwezi Septemba, mwaka huu.

Pendekezo hilo halikusema iwapo Iran haitafuata maagizo basi suala lake litapelekwa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Baraza hilo lina uwezo wa kuiwekea nchi hiyo vikwazo.

Lakini wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wamsema kama Iran haitafuata maagizo ya pendekezo hilo basi wataomba viongozi hao kupeleka suala hilo kwenye Baraza la Usalama.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Kofi Annan, amesema ifikapo mwezi Septemba na bado Iran na nchi za Magharibi hazitakuwa zimefikia makubaliano, badi wakati wa mkutano mkuu wa Umoja huo atawakutanisha viongozi wa nchi hizo kwa mazungumzo.

Viongozi wa ngazi za juu wa serikali za uingereza, Ufaransa na Ujerumani wamepanga kukutana na maafisa wa serikali ya Iran mwisho wa mwezi huu.

Bwana Annan katika mahojiano na shirika la habari la Reuters alisema ikiwa hawatakutana basi atatumia nafasi ya mkutano mkuu wa Umoja huo kuwakutanisha.

Umoja wa Mataifa utakuwa na mkutano mkuu mwezi ujao wa Septemba na Rais mpya wa Iran, Bwana Mahmoud Ahmadinejad, anategemewa kuhudhuria. Baada ya mkutano huo mkuu kutakuwa na mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje.

Ingawa Umoja wa Ulaya na Marekani uliiomba Iran isiendelee na mpango wake wa kinuklia, Nchi hiyo iliondoa vizuizi vilivyowekwa na wakaguzi wa Umoja wa Mataifa katika kiwanda cha Isfahan.

Iran ilisema mpango wake wa kutengeneza nuklia ni kwa ajili ya nishati kwa sababu kumekuwa na ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme. Wanataka kuuza mafuta na gesi nje ya nchi.

Nayo Iran imelikataa pendekezo hilo na kusema hawata litekeleza. Akizungumza na televisheni ya taifa ya Iran, kiongozi wa shirika la masuala ya nuklia wa nchi hiyo, Bwana Mohamaad Saeedi, amesema pendekezo hilo halifuati sheria za kimataifa kwa hivyo hawalazimiki kulitekeleza.

Aliongeza kwamba kazi katik akiwanda cha Isfahan itaendelea na nchi yake itaendelea kuwasiliana na shirika la masuala ya kinuklia la Umoja wa Mataifa. Pia Iran linawaruhusu wakaguzi wa Umoja huo kurudi Iran.

Bwana Elbaradei ana matumaini kwamba suala zima litasuluhishwa bila mgogoro kutokea.