1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IPCC - Kuna uhusiano kati ya matumizi ya ardhi na Tabia Nchi

8 Agosti 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kisayansi kuhusu mabadiliko ya tabia nchi IPCC katika ripoti yake mpya linaonyesha uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya ardhi na mabadiliko ya tabia nchi.

https://p.dw.com/p/3NXid
Burundi Landwirtschaft
Picha: picture alliance/africamediaonline

Ripoti hiyo inasema mabadiliko makubwa katika mfumo wa chakula ni muhimu sana kwa maisha na afya ya mamilioni ya watu.

Idadi ya watu duniani inazidi kuongezeka na hii inamaanisha kuwa matumizi pia yanaongezeka ila raslimali za dunia zina kikomo ardhi ikiwa mojawapo.

Wataalam 103 kutoka nchi 52 wameifanyia kazi ripoti hii kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili. Ripoti hii pia imejadiliwa na serikali mbalimbali kuanzia Agosti 2 hadi 6 mjini Geneva Uswisi na imeidhinishwa na nchi zote zinazoshiriki ambazo ni wanachama wa IPCC.

Mavuno duniani yanatarajiwa kupungua kutokana na Tabia Nchi

Ripoti hiyo haionyeshi mustakabali mwema kwani inasema kuwa iwapo kiwango cha joto duniani kitaongezeka zaidi ya kiwango cha nyuzi joto mbili kilichowekwa katika yale makubaliano ya Paris, uwezekano wa kitakachotokea ni kwamba ardhi yenye uwezo wa kuzalisha chakula itabadilika na kuwa jangwa, miundo mbinu itaharibika na ukame na hali mbaya zaidi ya hewa itauweka mpango wa chakula katika hali ya hatari.

Südafrika Dürre Totes Rind
Ukame na majangwa yataongezeka iwapo joto litazidi kiwango kilichowekwa ParisPicha: picture-alliances/dpa//K. Ludbrock

Mavuno yanatarajiwa kupungua kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na bei za chakula zinatarajiwa kupanda mno. Bei ya nafaka duniani inatarajiwa kuongezeka kwa hadi asilimia 23 kufikia mwaka 2050 kulingana na ripoi hiyo.

 Afisa wa shirika la Kimataifa linalohusika na masuala ya wanyama pori WWF Joao Campari anasema huenda mambo yakawa mabaya Marekani kulingana na ripoti ya awali ya idara ya ukulima nchini humo.

"Iwapo gesi chafu zitaendelea kutolewa uzalishaji wa maharagwe ya soya na mahindi nchini Marekani huenda ukapungua kwa hadi asilimia 80 katika miaka sitini ijayo," alisema Campari.

Ripoti hii si onyo tu bali mwito wa hatua kuchukuliwa

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa katika ardhi ya dunia ambayo haijafunikwa na barafu karibu asilimia sabini ya ardhi hiyo inatumika kwa uzalishaji wa chakula, nguo na mafuta. Inatumika pia kwa kuishi na matakwa mengine ya kibinadamu na yote haya yanachangia kwa karibu robo tatu ya gesi chafu zinazotolewa hewani. Kilimo kinachangia asilimia sabini ya idadi ya misitu inayokatwa duniani.

FAO - Verschwendung von Lebensmitteln
Asilimia kubwa ya chakula duniani huishia kutupwaPicha: FAO/Jonathan Bloom

Alisher Mirzabaev ambaye ni mmoja wa waliohusika katika uandishi wa ripoti hiyo ameiambia DW kuwa ripoti hiyo si onyo tu bali ni mwito wa hatua kuchukuliwa na kuukumbusha ulimengu kwamba bado kuna matumaini.

Ingawa suluhisho ni tofauti kulingana na kanda, kuna uhusiano. Joao Campari anasema suluhisho linaanza kwa kutumia vyema ardhi zilizopo kwa ajili ya uzalishaji wa chakula na kuzitia rotuba ardhi ambazo haziwezi kutumika katika masuala ya uzalishaji wa chakula.