1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

India yafanikiwa kupeleka chombo anga za juu kulitafiti Jua

6 Januari 2024

Chombo cha utafiti wa anga za mbali cha India kimefanikiwa leo kuingia kwenye mzingo wa Jua baada ya safari ya miezi minne ya kwenda kuifanyia utafiti nyota hiyo iliyozungukwa na sayari ikiwemo dunia.

https://p.dw.com/p/4avgh
Safari ya Aditya-L1
Roketi iliyobeba chombo cha anga za mbali cha India, Aditya-L1, iliporuka Septemba 2023.Picha: R. Parthibhan/AP Photo/picture alliance

Tangazo hilo limetolewa na waziri wa sayari na teknolojia wa India, Jitendra Singh, na kusifiwa na waziri mkuu wa taifa hilo Narendra Modi ambaye amesema mafanikio hayo ni "alama ya kihistoria" kwa India kwenye mradi wake wa anga za mbali.

Chombo hicho kilichopewa jina la Aditya -L1 kilirushwa mnamo mwezi Septemba na kimebeba vyombo vya kisasa vitakavyopima na kuchunguza tabaka la juu la Jua. Kimesafiri kiasi kilometa milioni 1.5 kutoka uso wa dunia umbali ambao ni asilimia moja pekee kutoka duniani hadi lilipo jua.

Mafanikio hayo yanaiweka India katika nafasi muhimu miongoni mwa mataifa machache duniani yaliyotuma vyombo vya anga za mbali kwenda kulitafiti Jua.