1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Ikulu ya White House yakosoa matamshi ya Trump dhidi ya NATO

11 Februari 2024

Ikulu ya Marekani, Jumamosi imeyakosoa matamshi yaliyotolewa na Rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump kuhusu kutowalinda washirika wa jumuiya ya kujihami ya NATO iwapo watakabiliwa na kitisho cha uvamizi wa Urusi

https://p.dw.com/p/4cGhU
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump akionyesha ishara wakati wa usiku wa uchaguzi mkuu wa urais huko Nashua, New Hampshire, Marekani, Januari 23, 2024
Rais wa zamani wa Marekani Donald TrumpPicha: Mike Segar/REUTERS

Siku ya Jumamosi, Trump alisema aliwahi kumweleza kiongozi wa taifa moja mwanachama wa NATO kuwa Marekani haitotoa ulinzi kwa mataifa yasiyotimiza wajibu wake wa kulipia kiwango cha bajeti cha kuendesha mfungamano huo wa kijeshi.

Soma pia:Trump aziwashia moto nchi za NATO

Vilevile amesema alieleza bila kificho kwamba  iwapo shambulio litatokea, atawahimiza wavamizi "kufanya wanavyotaka".

Matamshi hayo ya Trump yamezusha ukosoaji mkubwa kutoka kwa wanasiasa nchini Marekani.

Msemaji wa White house asema kuhimizia uvamizi kutahatarisha usalama wa Marekani

Akizungumzia matamshi hayo ya Trump, msemaji wa ikulu ya White House Andrew Bates, alisema kuhimiza uvamizi wa washirika wao wa karibu kutoka kwa kile alichokiita ''tawala za mauaji'' kunahatarisha usalama wa taifa wa Marekani, utulivu wa kimataifa na uchumi wa nchi hiyo.

Soma pia:Katibu Mkuu wa NATO kukutana na Donald Trump

Kupitia taarifa aliyotoa jana jioni, Bates ameongeza kuwa badala ya kuitisha vita na kuendeleza machafuko, Rais wa nchi hiyo Joe Biden ataendelea kuimarisha uongozi wa Marekani na kusimamia maslahi ya usalama wa kitaifa.