1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi ziongezwe

Angela Mdungu
15 Oktoba 2021

Shirika la kimataifa la nishati IEA limezitaka serikali duniani ziwajibike zaidi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi

https://p.dw.com/p/41jAq
BdTD Bild des Tages deutsch Grönland Gletscher Eisschmelze Klimawandel
Picha: Mario Tama/Getty Images

Shirika hilo la kimataifa la nishati limesema uwekezaji katika nishati mbadala utahitaji kuongezeka mara tatu kufikia mwisho wa muongo huu kama mataifa yanataka kufikia malengo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Shirika hilo, linaloshauri serikali juu ya sera za nishati, lilitoa ripoti yake ya hali ya nishati duniani Jumatano wiki hii, wiki chache kabla ya mkutano wa kilele wa mazingira COP26  utakaofanyika mjini Glasglow, Scotland.

Ripoti ya shirika hilo imetolewa huku bei za umeme zikipanda kwa kiwango kikubwa wakati masharti ya kukabiliana na virusi vya corona yakilegezwa kote ulimwenguni. Ripoti hiyo inayotolea kila mwaka hutoa mwelekeo wa matarajio kwa serikali, makampuni, na wawekezaji, juu ya matumizi ya baadaye ya makaa ya mawe, mafuta na gesi

Kwa muda mrefu, wakosoaji wamelikosoa shirika hilo kwa kutoipa uzito kasi ya namna dunia inavyobadilisha matumizi ya nishati kwenda kwenye nishati mbadala, hivyo kupunguza nguvu mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.

Awali, mashirika na wanaharakati wa mazingira walilituhumu shirika hilo la kimataifa la nishati kwa kuunga mkono uwekezaji wa mafuta ghafi. Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya mazingira ya Stocholm ameliambia shirika la utangazaji la DW kwamba, shirika hilo la IEA sasa limebadili mwelekeo na limewaomba viongozi kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi

Ripoti ya mwaka ya shirika hilo lenye makao yake mjini Paris imesema vyanzo vya nishati mbadala kama vile jua, upepo, umeme unaotokana na maji na nishati mbadala inayotokana na viumbe hai, vinapaswa kuwa sehemu kubwa katika kuongeza uwekezaji baada ya janga la virusi vya corona.

Ripoti hiyo imeonesha pia kuwa, mahitaji ya nishati mbadala yanaendelea kukua Hata hivyo imesema, mchakato wa nishati safi unakwenda taratibu kuliko kawaida katika kusaidia kupunguza hewa chafu duniani ili ifikie kiwango sifuri itakapofika mwaka 2050.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, zaidi ya asilimia 40% ya hewa chafu inayotakiwa kuondolewa itatokana na hatua zitakazojigharamia zenyewe kama vile, kuongeza ufanisi, kupunguza kuvuja kwa gesi au kuweka umeme wa jua ama upepo katika maeneo ambayo sasa teknolojia hizo zina ushindani zaidi katika uzalishaji wa umeme.

Yanayoweza kujitokeza

Ripoti hiyo pia ilichambua hali zinazoweza kujitokeza. Ya kwanza inaangazia hatua na sera ambazo serikali tayari zimeshazichukua. Licha ya hatua hizo, uzalishaji wa hewa chafu utaendelea kuwa katika kiwango kile kile wakati nchi zinazoendelea zikijenga miundombinu yao. Katika mazingira haya, kiwango cha joto katika mwaka wa 2100 kitakuwa asilimia 2.6 juu zaidi ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya ukuaji wa viwanda.

Mazingira ya pili yanaangazia ahadi za serikali kutaka kufikia kiwango sifuri cha uzalishaji wa gesi chafu, jambo linaloweza kuongeza uwekezaji wa nishati safi mara mbili  katika karne ijayo. Ikiwa mataifa yatatekeleza ahadi hizi kwa wakati, wastani wa ongezeko la kiwango cha joto duniani utakuwa karibu nyuzi joto 2.1 utakapofika mwaka 2100.

Ripoti hii ya wiki hii imetoa ishara ya kuzishinikiza serikali zichukue hatua zaidi wakati zikielekea katika mkutano wa kilele wa mazingira