1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliouawa katika shambulizi la Kabul wapindukia 100

Caro Robi
28 Januari 2018

Afghanistan imetangaza Jumapili kuwa siku ya maombolezi baada ya zaidi ya watu 100 kuuawa katika shambulizi la mabomu lililotokea katika mji mkuu wa Kabul siku ya Jumamosi lililosababisha pia majeruhi zaidi ya 200.

https://p.dw.com/p/2rfAU
Tag der Tauer in Afghanistan Kabul
Picha: Reuters/O. Sobhani

Shambulizi hilo la pili kutokea ndani ya wiki moja mjini Kabul linadaiwa kufanywa na wanamgambo wa Taliban. Watu 103 wameuawa na wengine 235 wamejeruhiwa huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka.

Mshambulizi wa kujitoa muhanga alijaza mabomu ndani ya gari la kuwabeba wagonjwa na kufanya shambulizi karibu na yaliyokuwa majengo ya wizara ya mambo ya ndani nchini humo.

Pia eneo hilo la shambulizi ni mita chache kutoka hospitali moja mjini Kabul ambako wengi wa wamejeruhi walipelekwa baada ya shambulizi hilo. Wengi wa waathiriwa walikuwa jamaa za wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya Jamhuriat.

Siku ya maombolezi yatangazwa na Serikali

Mji huo uko katika hali ya tahadhari, wakati ambapo Ikulu ya Rais imetangaza siku ya maombolezi na bendera kuagizwa kupeperushwa nusu mlingoti. Shambulizi hilo la Jumamosi ni mojawapo ya mashambulizi mabaya kuwahi kuukumba mji huo mkuu wa Afghanistan katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Afghanistan Explosion in Kabul
Askati akishika doria katika eneo la shambulizi mjini KabulPicha: picture-alliance/dpa/Zumapress

Mwezi Mei mwaka jana, karibu na ubalozi wa Ujerumani, watu 150 waliuawa na wengine 400 walijeruhiwa. Kuongezeka kwa mashambulizi nchini humo kumepelekea Marekani na Jumuiya ya kujihami ya NATO kuamua kuongeza idadi ya majeshi yake nchini humo.

Siku ya Jumapili mji huo wa Kabul uliko kimya, kinyume na ilivyo kwa kawaida ambapo Jumapili huwa ni siku ya kazi mjini humo. Idadi ndogo ya watu na magari meshuhudiwa katika mitaa ya mji huo.

Huku hayo yakijiri, tahadhari imetolewa kuwa kundi la wanamgambo wenye itikadi kali wa Dola la Kiislamu IS ambao walidai kuhusika katika shambulizi la Jumatano lililolenga ofisi za shirika la Save The Children wanapanga kushambulia maduka makubwa yanayotembelewa na raia wa kigeni.

Rais wa Marekani Donald Trump amateka hatua kali na madhubuti kuchukuliwa dhidi ya wanamgambo wa Taliban kufuatia shambulizi hilo la Jumamosi. Viongozi wengine wa kimataifa pia wamelaani shambulizi hilo.

Papa Francis awaombea Waafghani

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amelaani mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa nchini Afghanistan akiuliza ni hadi lini watu nchini humo watazidi kuteseka kutokana na ghasia na unyama.

Taliban Anschlag in Kabul
Raia na askari waliojeruhiwa wakiondoka eneo la shambuliziPicha: picture-alliance/dpa/M. Hossaini

Papa aliwaombea waathiriwa na familia zao na wale wote ambao wako nchini Afghanistan wakijaribu kuhakikisha nchi hiyo inapata amani.

Mkuu wa shirika la ujasusi la Afghanistan Mohammed Masoom Stanekzai amelitaja shambulizi hilo kuwa kisasdi Taliban inafanya kwa kushindwa katika mapambano na vikosi vya usalama na kukanusha kuwa kuna mapungufu katika jinsi usalama unavyoshughulikiwa nchini akisisitiza wametibua mashambulizi mengi lakini mengine ni magumu kuyadhibiti.

Wafghani wameelezea kusikitishwa kwao na hali ya usalama nchini mwao katika mitandao ya kijamii, wakilalamika kuwa ni vigumu kwao kuendelea na maisha yao ya kila siku kwa kuhofia kushambuliwa.

Serikali inayalaumu makundi ya kigaidi kama Taliban, mtandao wa Haqqani na IS kwa kuhusika katika misururu ya mashambulizi ya hivi karibuni mjini Kabul.

Mwandishi: Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Yusra Buwayhid